Ikiwa imebaki siku moja waumini wa dini ya Kikristo washerehekee sikukuu ya Christmas, wafanyabiashara wa masoko ya jiji la Dar es Salaam yakiwemo Kariakoo na Kisutu wamezungumzia hali ya biashara katika msimu huu.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Dar24, wafanyabiashara hao ‘wamelia’ na mdororo wa mauzo wakilinganisha na hali ilivyokuwa katika msimu kama huu katika miaka iliyopita.

Wamesema kuwa kwa kulinganisha na misimu ya miaka iliyopita, hali ya biashara mwaka huu imekuwa tofauti na walivyotarajia huku wengi wakidai huenda imetokana na hali ngumu ya maisha iliyoikumba mitaa kwa kipindi hiki.

Hata hivyo, baadhi ya wafanyabiashara hao wa nguo, kuku na vyakula wameeleza kuwa ingawa hali ni ngumu, wanapata riziki tofauti na nyakati nyingine za katikati ya mwaka.

“Biashara ya msimu huu wa Christmas ni tofauti kabisa na misimu iliyopita. Sio nzuri sana, pesa imekuwa ngumu. Kila mteja anayekuja hapa anakulalamikia pesa imekuwa ngumu,” alisema mfanyabiashara aliyejitambulisha kwa Gardena Alibibi.

Aidha, baadhi walidai kuwa kubanwa kwa watumishi wa umma kumechangia wao kutopata fedha kwani mzunguko wa fedha umepungua.

“Watu wa Serikalini wanapopata hela na sisi watu wa chini tunakuwa tunapata kidogo. Sasa watu wa Serikalini wanalia, unadhani sisi tutapata nini?”

Angalia video hapo chini upate undani na hali ilivyo masokoni Dar:


Anayetajwa kumvaa Pacquiao ajitangaza kuwa ‘bondia wa mwaka 2016’
Makonda apiga marufuku bomoabomoa Dar bila kigezo hiki