Vijana nchini wametakiwa kujijengea mazoea ya kupenda kujifunza kila wakati ili kuendelea kuibua mawazo endelevu kwa mustakabari wa maendeleo yao.

Hayo yamesemwa na Rais wa Jukwaa la Ujasiriamali Jamii Tanzania (TASEF) Adrian Nzamba wakati wa majadiriano ya Ripoti ya Hali ya Ajira iliyoandaliwa na Shirika la Kazi la Dunia (ILO) wakati wa majadiliano yaliyoandaliwa na Jukwaa hilo jana  Jijini Dar es Salaam.

“Vijana tunatakiwa tuwe na moyo wa kujifunza, wengi wetu wamekuwa wazito kujifunza” . Alisema Adrian.

Aliongeza kuwa kupitia Jukwaa hilo wamekuwa wakiwajengea uwezo Vijana katika hatua ya kujitambua na kuepukana na mawazo mgando yenye fikra hasi.

Kwa upande wake Meneja wa Buni Hub mshiriki mwenza wa Jukwaa hilo Jumanne Mtambalike ameipongeza Serikali kwa mchango wake katika kusaidia Vijana kufikia malengo yao.

Mtambalike amesema kuwa wao kama Buni Hub wamekuwa chini ya Tume ya Sayansi Tanzania (COSTECH) ambayo ni Taasisi ya Serikali hivyo ni dhahiri kuwa Vijana wakijitambua wanazo fursa nyingi kupitia Serikali yao kwani wao kama taasisi binafsi lakini wananufaika.

Aliongeza kuwa lengo kubwa la kushiriki Jukwaa hilo ni kuwajengea uwezo vijana wa kufikiri na kujitegemea badala kukaa na kulalamika bila sababu ya msingi.

“Vijana tumekuwa na tabia ya kulalamika sana, zipo fursa nyingi tu ili mradi unapata taarifa tafuteni taarifa zipo fursa nyingi sana binafsi nilipata udhamini wa kusoma nje ya nchi kupitia Wizara ya Habari kwa sababu nilitafuta taarifa”. Alisema Mtambalike.

Aidha alitoa rai kwa Taasisi za Elimu ya Juu kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuangaliana namna ya kuwa na njia bora ya kuwaandaa vijana ili kukidhi mahitaji ya soko la ajira.

Katika Jukwaa hilo vijana waliibua hoja mbalimbali zikiwemo kubadilisha mfumo  wa Elimu ili kuingiza mitaala ya Ujasiriamali, vijanga kujishughulisha na utafutaji wa taarifa na msisitizo wa vijana kushiriki katika kazi za kujitolea.

Serikali Kuboresha Ufundishaji Shule Za Awali,Msingi Na Sekondari
Prof.Muhongo Awapa Neno Wanafunzi Waliopata Ufadhili Wa Masomo Ya Mafuta Na Gesi