Viongozi wakuu wa chama cha Republican wamezidi kuondoa uungaji mkono kwa Donald Trump mara baada ya video iliyovuja ya matamshi yake ya kuwadhalilisha wanawake
Miongoni mwa wanasiasa hao ni pamoja na aliyekuwa waziri wa mambo ya nje wa Marekani Condoleezza Rice, na aliyegombea kiti cha urais nchini humo, Senator John McCain.
Kwa upande wake Trump ameendelea na msimamo wake wa kutojitoa katika kinya’anyiro cha kuwania kiti hicho licha ya malalamiko kutoka kote duniani kutokana na matamshi yake ya kuudhi kwa wanawake, aliyo-yatoa mwaka 2005.
Zaidi ya wanasiasa 24 wa chama chake cha Republican, sasa wamesema hawana imani naye na hawamuungi mkono bilionea huyo na wanamtaka kumuachia mgombea mwenza Mike Pence nafasi ya kuwania kiti cha Urais katika uchaguzi mkuu wa Marekani hapo mwezi Ujao.
Miongoni mwa wanaolaani matamshi hayo ya Trump ni pamoja na mkewe Trump- Melania, amesema kuwa licha ya kuendelea kumuunga mkono lakini analaani matamshi hayo dhidi ya wanawake.
Spika wa Bunge Paul Ryan, alizomewa na kushangiliwa kwa wakati mmoja, katika mkutano mmoja wa kisaiasa baada ya kukataa kutumia jukwaa moja na Bwana Trump.