Wabunge nchini Rwanda wamepitisha muswada wa sheria unaompa nguvu Rais wa nchi hiyo kuunda na kufuta makampuni na mashirika ya Serikali.

Muswada huo ulipitishwa bungeni kwa kupata kura 78 za ndio na kura 2 tu za hapana, hivyo kuufanya uwasilishwe kwa ajili ya kusainiwa na Rais na kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali kuwa sheria kamili.

Uamuzi huo wa Bunge umetokana na Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya Mwaka 2019 kuonesha madhaifu na ubadhirifu kwenye makampuni mengi na taasisi za Serikali.

Ripoti hiyo imeeleza kuwa asilimia 31 ya taasisi na makampuni ya Serikali hayakupata hati safi katika ukaguzi huo. Makampuni mengine yalionekana kusababisha hasara kwa miaka kadhaa mfululizo.

“Taasisi za Serikali kama Wasac ambazo zinawezeshwa ili kutoa huduma, bado zinafanya kazi kwa hasara. Nini kinazizuia kufanya kazi kama taasisi zinazotoa faida?” CAG, Obadiah Biraro aliuliza.

 Hivyo, wabunge wanaamini kuwa kumpa nguvu Rais kuziunda na kuzifuta taasisi hizo kutasaidia kuongeza ufanisi na uadilifu.

Waliounga mkono muswada huo wameeleza kuwa hatua hiyo itasaidia kuondoa ukiritimba katika kuyashughulikia makampuni yaliyosababisha hasara, kwa kusubiri hoja ziwekwe bungeni na kutafuta sababu.

Ajira: Makampuni 10 yatangaza nafasi za kazi, ziko hapa
Magufuli awapa mtihani mzito wateule wake wanaotaka Majimbo 2020 "Tamaa ya madaraka"