Wachimbaji wa Madini Kanda ya Ziwa na maeneo ya jirani wametakiwa kutumia huduma za utafiti, ushauri elekezi, uchambuzi wa sampuli kupitia maabara za GST zilizopo katika ofisi mpya iliyofunguliwa ili wachimbe kwa tija.

Rai hiyo, imetolewa na Waziri wa Madini, Doto Biteko leo Septemba 21, 2021 wakati akifungua jengo la Kituo cha Ofisi ya Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) mkoani Geita kwa ajili ya kutolea huduma.

Waziri Biteko amesema, Shughuli za utafutaji wa Madini ni sayansi, hivyo wachimbaji watumie sayansi katika kutafuta Madini.

“Tuwatumie wataalam ambao nchi imewasomesha kwa gharama kubwa ili waweze kusaidia kupata taarifa sahihi za miamba na uwepo wa madini katika maeneo tunayofanyia kazi,” amesema Waziri Biteko.

Amesema, GST imeona ni muhimu kusogeza huduma ya ofisi karibu na maeneo ya wachimbaji ili kuwaweka karibu na watendaji.

“Nataka niwahakikishieni, tukio hili ni mwanzo wa mambo mengi ambayo Sekta ya Madini itafanya kwenye Mkoa wa Geita,” ameongeza Waziri Biteko.

Kwa upande mwingine, Waziri Biteko amesema, ujenzi wa jengo la ofisi ya Madini ya kisasa lenye thamani ya shilingi bilioni 4 na milioni 500 unaanza hivi karibuni ili huduma zitolewe karibu.

Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila amesema, Serikali na Wizara ya Madini imekuwa ikiwezesha GST ili iweze kuimarisha miundombinu ya kutoa huduma yao.

Prof. Msanjila amesema, kusogeza Kituo cha GST katika Mkoa wa Geita unalenga kuwawezesha wachimbaji katika kuchangia kikamilifu Pato la Taifa kupitia Shughuli za uchimbaji madini.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa GST, Dkt. Mussa Budeba, amesema, ofisi ndogo iliyozinduliwa na Waziri Biteko pamoja na ofisi zitakazojengwa sehemu mbalimbali zitatoa mafunzo kwa wachimbaji wadogo ya namna ya uchukuaji sampuli ili kuwajengea uwezo wa kuchimba kwa tija.

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Septemba 23, 2021
Mikoa 6 yakabidhiwa magari yenye thamani ya milioni 646.