Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania ‘TFF’ Wallace Karia amezitaka klabu za Simba SC, Young Africans, Geita Gold na Azam FC kujiandaa vizuri kwa ajili ya Michuano ya Kimataifa inayoratibiwa na CAF, itakayoanza rasmi mwezi Septamba.

CAF ilitangaza ratiba ya michezo ya awali ya Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika na Kombe la Sirikisho Barani humo juzi Jumanne (Agosti 09), huku Klabu ya Azam FC ikipata nafasi ya kuanzia Mzunguuko wa kwanza kwenye Michuano ya Kombe la Shirikisho.

Karia amesema Klabu za Tanzania zinapaswa kuwa makini katika maandalizi yao, ili kuwa na ushiriki mzuri kwenye Michuano hiyo ya Kimataifa.

“Klabu zinatakiwa kujiandaa kwa ajili ya Michuano ya Kimataifa kwa sababu ushindani umeongezeka, nina uhakika tuna timu nzuri zinazoweza kupambana, hivyo ninawasihi viongozi na wachezaji kujiandaa vizuri.”

“Tanzania imepata heshima ya kupeleka timu nne kwenye Michuano ya Kimataifa, ili kuendelea kutetea nafasi hizi, Klabu zetu zinatakiwa kupambana na kufika katika hatua za juu.” amesema Karia

Katika hatua nyingine Karia amepiga marufuku tabia ya baadhi ya Mashabiki wa Soka nchini kuzipokea na kuzishangilia timu za kigeni, pindi zinapokuja nchini kucheza Michuano ya Kimataifa.

“Ni vizuri zile tabia za kupokea na kushangilia wageni zikafa, maana hakuna tunayemkomoa zaidi ya kujikoa sisi wenyewe kama nchi.” amesisitiza Karia.

Timu ya Simba itakutana na Nyasa Big Bullets Fc ya Malawi huku Young Africans ikikutana na Zalan FC ya Sudan Kusini katika michezo ya hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.

Mshindi wa mchezo kati ya Simba Vs Nyasa Big Bullets atakutana na mshindi kati ya Red Arrors ya Zambia Vs Premeiro de Agosto ya Angola katika hatua ya pili kabla ya kutinga hatua ya Makundi.

Mshindi kati ya Young Africans Vs Zalan atakutana na mshindi kati ya St. George Sc ya Ethiopia Vs Al Hillal ya Sudan katika hatua ya pili kabla ya kutinga hatua ya Makundi.

Kwa upande wa Geita Gold Fc watakutana na Hilal Al Sahil ya Sudan katika hatua ya awali ya Kombe la Shirikisho CAFCC, na mshindi wa hatua hiyo atakutana na Pyramid ya Misri.

Simba SC yaomba radhi hadharani
Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Agosti 11, 2022