Jumla ya Watu 11, wakiwemo Polisi wawili wamefariki Dunia kufuatia ajali ya mkanyagano uliotokea kwenye tamasha la Stampede la msanii wa muziki wa miondoko ya kilingala, Fally Ipupa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC.

Tukio hilo limetokea Oktoba 30, 2022 katika Uwanja wa Martyrs uliopo jiji la Kinshasa, ikidaiwa kuwa uwanja huo ulijaa kupita uwezo wake na baadhi ya umati wa watu uliishia kulazimisha kuingia kwenye ukumbi wa VIP na sehemu zilizotengwa.

Mamlaka sa usalama nchini humo, zimesema watu wengi walikufa kwa kukosa pumzi wakati wa mkasa huo wakati msanii huyo maarufu akifanya tamasha katika uwanja huo mkubwa wenye uwezo wa kupokea watu 80,000.

Aidha, mashuhuda wa tukio hilo, wakisimulia wamesema uwanja huo ulijaa kupita kiasi na Polisi walishindwa kuuzuia umati wa watu waliokuwa wamekusanyika nje ya uwanja huo.

Sehemu mojawapo ambayo uharibifu wa mageti ulitokea baada ya watu kulazimisha kuingia kwa nguvu uwanjani. Picha: Reuters.

Awali, Polisi walifyatua mabomu ya machozi kujaribu kutawanya umati wa watu wenye vurugu nje ya uwanja, ambapo wengi walikuwa wamekusanyika kabla ya tamasha kuanza.

Mwaka 2020, vurugu zilizuka mjini Paris nchini Ufaransa kabla ya tamasha la Fally Ipupa (44), ambaye ni mzaliwa wa Kinshasa na ni mmoja wa wanamuziki mashuhuri barani Afrika, ambaye ana umaarufu kote ulimwenguni.

Hassan Dilunga afunguka ya moyoni
Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Octoba 31, 2022    Â