Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James amewaonya watendaji wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wanaojihusisha na vitendo vya ukosefu wa maadili vinavyochangia kuikosesha serikali mapato yake yatokanayo na kodi, vikiwemo vitendo vya rushwa kuwa watachukuliwa hatua hatua kali.

Ameyasema hayo wakati akihitimisha kikao maalum kati ya Menejimenti ya Wizara ya Fedha na Mipango, Wajumbe wa Bodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, pamoja na Mameneja wa Mikoa yote ya Tanzania Bara wa Mamlaka hiyo.

Amesema kuwa vitendo vinavyofanywa na baadhi ya watumishi wa Mamlaka hiyo ikiwemo vitisho kwa wafanyabiashara wakati wa kukusanya kodi havikubaliki na kwamba Serikali ya awamu hii imejipanga kukabiliana na vitendo hivyo kwa nguvu zote hivyo watakaobainika watachukuliwa hatua kali za kinidhamu ikiwemo kufukuzwa kazi.

Aidha, mpaka sasa tayari wafanyakazi kadhaa wa Mamlaka hiyo wamefukuzwa kazi huku wengine wakihamishwa vituo vyao vya kazi kutokana na mwenendo wao usioridhisha na kulalamikiwa kutofuata maadili yao ya kazi wakati wanatekeleza majukumu yao.

Hata hivyo, Katibu Mkuu huyo ameiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, kuhakikisha kuwa inafikia malengo ya kukusanya kiasi cha shilingi trilioni 18 katika mwaka huu wa Fedha wa 2018/2019, ikiwa ni sehemu ya Bajeti ya shilingi trilioni 32.47, iliyopitishwa na Bunge.

 

Zoezi la uhakiki wa leseni lasitishwa
Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Agosti 4, 2018