Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameungana na wakuu wa nchi na viongozi mbalimbali 700 kutoka nchi 195 na mashirika ya kimataifa 23 kuweka mashada kwenye mazishi ya kitaifa ya Waziri Mkuu mstaafu wa Japan, Shinzo Abe.

Majaliwa, amemuwakilisha Rais Samia kutoa heshima hizo za mwisho hii leo (Septemba 27, 2022) kwenye ukumbi wa Nippon Budokan akiwa ameambatana na mkewe Mary Majaliwa, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassoro Mbarouk, Balozi wa Tanzania nchini Japan, Balozi Baraka Luvanda na mkewe Consolata Luvanda.

Baada ya kutoa heshima za mwisho, Waziri Mkuu alikwenda kwenye Kasri la Kifalme la Akasaka, jijini Tokyo ambako hufanyika shughuli zote za Kiserikali, ili kumfariji Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Fumio Kishida pamoja na mjane wa Shinzo Abe, Akie Abe.

Akie Abe, mke wa Waziri Mkuu wa zamani Shinzo Abe, aliyeketi kulia, anaonekana kwenye gari la kubeba mwili wa Abe wakati ikitoka kwenye hekalu la Zojoji Julai 12, 2022. Abe aliuawa alipokuwa akifanya kampeni huko Nara, magharibi mwa Japani. (Picha na Kyodo News / AP)

Viongozi wengine wa kitaifa walioshiriki mazishi hayo ni Marais kutoka Vietnam, Sri Lanka, Makamu wa Rais kutoka Indonesia, Marekani, Ufilipino, Marais wastaafu wa Ufaransa, Ujerumani na Mfalme wa Falme za Kiarabu, mtawala wa Qatar na Amiri wa Kuwait. Mawaziri Wakuu 16 walihudhuria mazishi hayo.

Mawaziri wakuu waliokuwepo ni Narendra Modi (India), Justin Trudeau (Canada), Han Duck-soo (Korea Kusini) na Antony Albanese (Australia). Wengine ni Mawaziri Wakuu wastaafu, Maspika, Majaji, wakuu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mabalozi. Baadhi ya nchi na taasisi zilizowasilisha salamu za rambirambi, zilisomwa majina yao.

Mapema asubuhi, wakazi wa Japan walijipanga kwenye misururu mirefu ili kupata fursa ya kutoa heshima zao za mwisho kwa kuweka mashada ya maua kwenye eneo maalum lililoandaliwa katika bustani nje ya ukumbi huo. Ukumbini kulikuwa na watu wapatao 4,300.

Kenya: Minong’ono yatawala Mawaziri wapya wa Ruto
Wizara ya Afya yathibitisha vifo 23 vya Ebola