Waziri wa Biashara, Viwanda na Uwekezaji, Charles Mwijage ameweka jiwe la msingi kwenye kiwanda cha Vigae cha Twyford Ceramics Ltd kilichopo katika kitongoji cha Pingo Chalinze, Bagamoyo.
Waziri Mwijage amezitaka taasisi zinazohusika na uwekezaji kutokuwa na ukiritimba ili hali kufikia malengo ya Serikali ya kukuza sekta ya viwanda. Aidha ameeleza kwamba, wizara hiyo imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji ambayo yatawezesha kuvutia wawekezaji wa ndani na nje.
Amesema kuwa uwekezaji huo unaendana na dhana ya Rais Dkt. John Magufuli wa kuifanya nchi kuwa ya Viwanda.
Amesema kwa kuanzishwa viwanda vingi vya aina hiyo kutasaidia kuongeza pato la nchi na kuzalisha ajira kwa wingi. “Zipo idara ambazo zinafanikisha uwekezaji ikiwemo brela, idara ya uhamiaji, kazi, mamlaka ya mapato TRA, wizara ya ardhi, shirika la viwango TBS, baraza la Mazingira NEMC ambazo zinapaswa kufanya kazi kwa wepesi ili kufanikisha uwekezaji,” alisema Mwijage.
“Wizara yangu haina tatizo lakini kuna baadhi ya idara zimekuwa kero na ukiritimba usio na sababu .,naomba kama kuna idara zinakuwa kikwazo niambieni ili tuwachukulie hatua,” alisema Mwijage.
Waziri Mwijage pia ameeleza kuwa nchi zilizofanikiwa kukuza uchumi wake kupitia viwanda zimeweza kutoa ajira nyingi kwa vijana kupitia sekta rasmi na isiyo rasmi.
Kwa upande wake Mkurugenzi mkuu wa kiwanda hicho, Jack Feng amesema kuwa kiwanda hicho asilimia 95 ya malighafi itakuwa inatoka nchini ambapo kigae kinatumia maliaghafi zaidi ya 10.
Amesema mara kiwanda hicho kitakapokamilika agosti mwaka huu kitaweza kupunguza asilimia 30 ya uagizaji wa vigae toka nje ya nchi.
Feng alisema wanatarajia kuajiri wafanyakazi 2,000 moja kwa moja na 4,000 kazi za muda na gharama ya mradi huo ni dola mil. 56 sawa na bil. 120 .
Pia Mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia, Evarist Ndikilo amesema mkoa huo una viwanda 264 huku vikubwa vikiwa ni viwili.
Amesema uwekezaji huo ni mkubwa na unatarajia kukuza ajira kwa vijana wa mkoa wa Pwani na Tanzania kwa ujumla, amesema mkoa wa Pwani bado una maeneo makubwa ya uwekezaji na tayari kuna eneo lenye ukubwa wa hekari 5,000 linahitaji wawekezaji .
Naye Mbunge wa Jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete amewapongeza wawekezaji hao kutoka nchi ya China, amesema Chalinze imejipanga kuwa sehemu ya uwekezaji ambapo kuna ujenzi wa viwanda mbalimbali.
Ameeleza kuwa changamoto kubwa inayokabiliwa wananchi na wawekezaji ni ukosefu wa maji,.
Alibainisha wamekuwa wakijitahidi kuikabili lakini bado hawajafanikiwa kuidhibiti aliomba wawekezaji hao kutoa ajira bila ya kuwabagua wenyeji.

Rais mstaafu, Kikwete akutana na Rais Outtara wa Ivory Cost, wazungumzia hali ya elimu Afrika
Trump apiga marufuku baadhi vyombo vya habari kuingia Ikulu ya Marekani