Kada mpya wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Wema Sepetu ametoa ujumbe mzito kwa mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema baada ya jana Mahakama kuamuru aachiwe kwa dhamana.

Lema alikaa mahabusu miezi minne baada ya upande wa Serikali kuwasilisha pingamizi la dhamana yake, pingamizi ambalo waliamua kuliondoa mahakamani katikati ya juma hili.

Jana, Wema alitumia mtandao wa Instagram wenye wafuasi zaidi ya milioni 2.6 kuandika ujumbe wa aina yake kwa Lema akimuahidi kufika jijini Arusha leo kwa lengo la kumtia moyo.

“Mungu ni mkubwa….Ni furaha kusikia Mh. Godbless Lema amepewa dhamana….Najua ulipitia wakati mgumu sana, najua ulikuwa mbali na familia yako, watoto wako, rafiki zako, makamanda wenzako na zaidi wananchi wako wa Arusha na Watanzania kwa ujumla….Ni faraja kwetu kwamba sasa umerudi mtaani kuendeleza mapambano…. Kwenye mapambano haya hautakuwa mwenyewe; Mdogo wako Wema nitakuunga mkono mpaka kieleweke….For that sake, Kesho i’ll be in Arusha kuonyesha Solidarity,” aliandika.

“For to be free is not merely to cast off one’s chains, but to live in a way that respects and enhances the freedom of others” – Nelson Mandela #callmekamanda” Aliongeza kwa herufi kubwa.

Hivi karibuni, Wema alitangaza kuihama CCM na kuhamia Chadema kwa kile alichodai kuwa ameenda kupigania demokrasia. Mrembo huyo alichukua uamuzi huo baada ya kutoka selo za polisi alikokuwa akishikiliwa kwa tuhuma za dawa za kulevya.

Mrembo huyo anakabiliwa na kesi ya matumizi ya dawa za kulevya na anatetewa na mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu.

Video: Polisi Rukwa wakamata Heroin na Scania lililosheheni pombe za viroba
Rais Dkt. Magufuli aagiza Mkandarasi anyang'anywe paspoti ya kusafiria