Hatima ya mabingwa wa soka Tanzania bara, Young Africans ipo mikononi mwa Shirikisho la Soka duniani (FIFA) baada ya Shirikisho la Soka nchini TFF kuwasilisha utetezi wa klabu hiyo hapo jana.

Afisa Habari wa TFF, Alfred Lucas alisema kuwa tayari Young Africans kupitia kwa katibu wao Baraka Deusdetit waliwasilisha utetezi wao na TFF kuutuma FIFA na kwamba kwa sasa suala hilo halipo mikononi mwao tena.

Katika utetezi huo, Yanga wanadai kuwa mtandao ulikuwa unasumbua kitu ambacho kiliwafanya wachelewe kuwasilisha usajili wao.

“Hatima yao (Yanga) ipo FIFA, sisi halipo kwenye mikono yetu tena, wamewasilisha utetezi wao tumeutuma, FIFA ndio wataamua kwa kuwa ndio yenye mamlaka ya kufungua dirisha,” alisema.

Iwapo FIFA haitaridhishwa na utetezi huo wa Yanga na kuutupilia mbali basi klabu hiyo itashushwa daraja ngazi ya Wilaya ambayo haipo kwenye usajili wa mfumo wa TMS.

Dirisha la usajili kwa timu zinazoshiriki Ligi Kuu ya Bara, Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Daraja la Pili msimu wa mwaka 2016/2017 lilifungwa saa 6.00 usiku wa Jumamosi Agosti 6, 2016.

Hadi dirisha linafungwa, timu za Young Africans na Coastal Union pekee ndio zilikuwa hazijawasilisha usajili wake licha ya kukumbushwa mara kadhaa na uongzi wa TFF.

Hata hivyo, katibu wa Young Africans alisema tayari wameshapeleka usajili wao juzi na afisa habari wa TFF Lucas amethibitisha hilo na kwamba wameshautuma FIFA lakini kama utakubaliwa ama la, ni juu ya shirikisho hilo la kimataifa.

Usajili wa msimu huu ni kama msimu uliopita kwamba unafanyika kwa njia au mfumo wa mtandao unaoitwa Transfer Matching System (TMS) ambao (server) yake au chombo chake cha kutunza kumbukumbu kipo mjini Zurich yalipo makao makuu ya FIFA.

Kwa kawaida mfumo huu upo chini ya FIFA na TFF hutoa taarifa kwa FIFA tarehe ya kufungua dirisha la usajili na kufunga. Mfumo huu unahusisha pande tatu ambazo ni klabu, shirikisho (TFF) na FIFA.

Kimsingi, kazi ya usajili hufanywa na klabu ambayo inajaza fomu kwa njia ya mtandao na hupakia viambatanisho kama vile mikataba na picha za wachezaji. Zoezi hili hufanywa na Meneja Usajili wa klabu husika wakati shirikisho hufanya kazi ya kuhakiki na kuidhinisha FIFA ambao husimamia mfumo mzima.

Simba SC Watoa Ufafanuzi Kuhusu Usajili Wa Mavugo
Rio Olimpiki 2016: Rekodi Iliyodumu Kwa Miaka 48 Yavunjwa