Mabingwa wa soka Tanzania bara Young Africans wmekamilisha mechi za mzunguko wa kwanza wa Kundi A Kombe la Shirikisho Afrika bila ushindi, kufuatia kulazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Medeama ya Ghana jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Matokeo hayo yanaifanya Young Africans iokote pointi ya kwanza, baada ya awali kufungwa 1-0 mara mbili mfululizo na MO Bejaia nchini Algeria na TP Mazembe ya DRC Dar es Salaam pia.

Young Africans inaendelea kukamata mkia kwenye kundi lake, wakati Medeama inabaki nafasi ya tatu kwa pointi zake mbili, nyuma ya MO Bejaia yenye pointi nne na TP Mazembe pointi sita.

Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Ibrahim Nour El Din, aliyesaidiwa na washika vibendera Ayman Degaish na Samir Gamal Saad wote wa Misri, hadi mapumziko tayari timu hizo zilikuwa zimefungana bao 1-1.

Young Africans walitangulia kwa bao zuri la mshambuliaji Donald Dombo Ngoma dakika ya pili, aliyemalizia pasi ya Mzimbabwe mwenzake, Thabani Kamusoko kumchambua kipa Daniel Adjei.

Baada ya bao hilo, Young Africans walisukuma mashambulizi zaidi langoni mwa Medeama, lakini hawakubahatika kuongeza bao.

Medeama wakafanikiwa kuiteka safu ya kiungo na kuanza kutawala mchezo, hatimaye kupata bao la kusawazisha dakika ya 17, mfungaji Bernard Donso akimalizia kona ya Enock Atta Adjei.

Kutoka hapo, timu hizo zikaanza kushambuliana kwa zamu hadi kipyenga cha kuhitimisha ngwe ya kwanza kilipopulizwa.

Kipindi cha pili, Medeama walikianza vizuri na kuendelea kutawala mchezo, lakini safu ya ulinzi ya Young Africans iliyoongozwa na Nahodha Vincent Bossou ilisimama imara.

Mashambulizi ya Young Africans hayakuwa ya kushitua langoni mwa Medeama na mshambuliaji Mrundi, Amissi Tambwe alionekana kabisa kujilazimisha kucheza akitoka kuugua Malaria.

Almanusra Medeama wapate bao la ushindi dakika ya 90 na ushei baada ya shambulizi la kushitukiza wakitoka kushambuliwa baada ya Abbas Mohamed kupiga mpira uliookolewa na Nahodha Vincent Bossou ukiwa unaelekea nyavuni.

Kikosi cha Young Africans kilikuwa; Deogratius Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Oscar Joshua/Juma Mahadhi, Kelvin Yondani, Mtogo Vincent Bossou, Mbuyu Twite, Thabani Kamusoko, Simon Msuva, Obrey Chirwa, Amissi Tambwe/Haruna Niyonzima dk na Donald Ngoma.

Medeama FC; Daniel Adjei, Samuel Adade, Moses Sapong, Paul Adoo/Salufu Moro dk62, Daniel Amouah, Kwesi Donsu, Erick Kwakwa, Kwame Boahene, Abbas Mohamed, Bernard Ofori na Enock Atta Agyei/Malik Akowuah dk79.

Bavicha watangaza kukutana tena Dodoma kivingine
Rais Magufuli amteua Mrema, atimiza ahadi ya kumpa Kazi