Jumla ya ombaomba sitini (60) wamekamatwa katika msako wa ombaomba unaoendelea katika jiji la Dar es Salaam.

 

Hayo yamesemwa leo na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Grace Magembe alipokuwa  akitoa majibu ya uwepo wa ombaomba katika jiji la Dar es Salaam licha ya kuwepo kwa operesheni ya kuwaondoa.

“Zoezi la ukamataji wa ombaomba katika jiji la Dar es Salaam linaendelea na ombaomba sitini wamekamatwa na kufunguliwa mashtaka, wakiwemo watoto wenye umri wa chini ya miaka 18 ambao wamepelekwa katika vituo vya watoto yatima kikiwemo kituo cha Kurasini,” alifafanua Dkt. Magembe.

Dkt. Magembe alisema kuwa bado ombaomba wamekuwa wakionekana ndani ya Jiji la Dar es Salaam kutokana na kuwepo kwa watu wanaotoka mikoani na kuingia katika makundi ya ombaomba kila siku.

Aidha, aliendelea kwa kusema kuwa kutokana na kuwepo na ongezeko kubwa la watu wanaotoka mikoani na kujiingiza katika makundi ya ombaomba, uongozi wa mkoa wa Dar es Salaam unashirikiana na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kutoa elimu mikoani juu ya operesheni ya kuondoa ombaomba katika jiji la Dar es Salaam wanaosababishwa na watu wanaokuja kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.

Mapema Aprili mwaka huu, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Paul Makonda alitangaza oparesheni kubwa ya kuondoa ombaomba katika Jiji la Dar es Salaam, ambapo alilitaka Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Ustawi wa Jamii kufanya zoezi la kuwaondoa ombaomba wote waliopo Jijini humo.

Aidha, Mhe. Makonda amepiga marufuku wananchi wanaotoa fedha kwa ombaomba  kuacha mara moja ili wajitafutie fedha wao wenyewe aidha kwa kufanya biashara au kurudi mikoani na kujishughulisha na Kilimo

Rwanda Yagomea Ombi la ICC Kumkamata Bashir
Waziri Mpina Apiga Faini Kampuni Ya Kanji Llji Na Prime Liberty Limited Kwa uchafuzi Wa Mazingira