Shirika la kimataifa la kudhibiti nguvu za Atomiki (IAEA), limeanza ukaguzi nchini Ukraine kama sehemu ya uthibitisho huru juu ya madai ya Serikali ya Urusi kuwa Kyiv inatengeneza mabomu machafu.
Kwa mujibu wa taarifa ya IAEA iliyotolewa Jumatatu ya Oktoba 31, 2022 imesema wataalamu wake tayari wameanza ukaguzi na wanatarajia kumaliza muda mfupi ujao shughuli za kuthibitisha madai hayo kwenye maeneo mawili nchini Ukraine.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa shirika hilo, Rafael Grossi anatarajia kutoa hitimisho la awali kuhusiana na kile kilichoonekana katika maeneo hayo ili kupata taswira halisi na kuelekeza taratibu za kufuata iwapo kuna ukweli.
Serikali ya nchi ya Urusi inayoongozwa na Rais Vladmir Putin, inaishutumu Ukraine kwa kujiandaa kutumia mabomu hayo dhidi ya wanajeshi wake, huku Kyiv ikihisi kwamba Urusi ndiyo inayotaka kutumia mabomu hayo.