Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Allan Kijazi amewataka wadaiwa sugu wa kodi ya Pango la Ardhi kulipa kodi hiyo kabla ya Serikali kuanza kuchukua hatua za kisheria ikiwemo wahusika kupoteza milki ya ardhi zao.
Dkt. Kijazi ameyasema hayo hii leo tarehe 4, Novemba 2022 Jijini Arusha wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha wasimamizi wa kodi wa Wizara ya Ardhi kutoka mikoa yote nchini kujadili namna bora ya ushirishaji wa makusanyo ya kodi ya pango la Ardhi.
Amesema, suala la kulipa kodi ya ardhi ni la kisheria hivyo kuwataka wananchi wote kuzingatia matakwa ya kisheria kwa kulipa kodi hiyo na kuwakumbusha kuwa Serikali imetoa msamaha wa riba kwa walipa kodi sugu na mwisho wa msamaha huo ni Disemba mwaka huu.
Aidha, amesisitiza Taasisi za Umma kuona ya haja ya kulipa kodi ya pango la ardhi kwani kwa sasa malimbikizo hayo yanazihusisha pia taasisi za umma na binafsi na uzoefu unaonesha kiwango kinachokusanywa kidogo kulinganisha na uhalisia kwa idadi ya walipa kodi.