Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam linawashikilia watu nane akiwemo mtangazaji wa Clouds, Shafii Dauda na mshereheshaji Mc Luvanda kwa kesi ya kumiliki na kuendesha blogu bila ya kibali ambacho walitakiwa kulipia Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Wengine ambao wanashikiliwa ni Tumaini Makene ambaye anaendesha blogu ya Chadema, Fadhili Kondo ambaye ni meneja wa msanii wa kizazi kipya Maua Sama, meneja wa Shetta Michael Mlingwa (Mx Carter) pamoja na Ben On Air ambaye anaendesha TV mtandaoni ya Shafii kupitia mtandao wa You Tube.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema ana taarifa ya kukamatwa kwa watu hao lakini kama wataongezeka atatoa taarifa rasmi muda utakapofika.

“Katika ofisi yangu yapo hayo majina nane kwa tuhuma za kuendesha blogu bila ya kuwa na kibali ambacho walitakiwa kulipia ili kuwa na haki ya kutumia na kuendesha,” alisema Mambosasa.

Aidha, mnamo April 21, 2018 TCRA ilitangaza rasmi kuanza usajili wa blogu, TV na Redio mtandaoni ambapo wamiliki wa vyombo hivyo vya habari wanatakiwa kulipia fedha kwa ajili ya usajili.

Usajili huo ni kwa mujibu wa kanuni ya 4 ya maudhui mtandaoni ya mwaka 2018 (The Electronic Postal Communication (Online Content) of 2018) ambapo TCRA imepewa dhamana ya kutunza na kuandaa rajisi ya watoa huduma za maudhui kupitia Blogu, majukwaa mtandaoni na kuchukua hatua kunapotokea ukiukaji wa kanuni tajwa na pia kueleimisha umma kuhusu kanuni hizo.

Mbowe: Siwezi kujiuzulu kwa shinikizo la CCM
Wolper aingilia kati sakata la Maua sama na Soudy brown kuwekwa rumande