Mchezea santuli na mtayarishaji wa muziki ambaye ni mmoja kati ya waasisi wa muziki wa Bongo Flava, Boniventure Kilosa aka Dj Boni Love amezungumzia mabadiliko yaliyopo kwenye uzio wa muziki huo pamoja namna watangazaji wanavyofanya kazi zao.

Mkongwe huyo amesema kuwa kilichobadilika hivi sasa, cha kwanza ni kwamba enzi zao wakati muziki wa Bongo Flava unaanza kushika hatam, watangazaji wa redio walikuwa wanazunguka studio kutafuta nyimbo. Lakini sasa hivi, wasanii na watayarishaji wa muziki wanalazimika kuandaa bajeti ya kusambaza nyimbo zao kwenye vituo vya redio na televisheni.

“Unajua zamani tulikua tunafanya kazi na presenters ndio walikua wanatafuta kazi kutoka kwetu sisi, lakini kwa sasa lazima uandae bajeti,” Boni Love aliiambia Ice FM.

Akizungumzia tasnia ya utangazaji wa vipindi vya burudani, nguli huyo alimtaja mtangazaji wa Times Fm, Omary Tambwe aka Lil Ommy wa 100.5 Times Fm kuwa ni mtangazaji anayejituma, mbunifu na kwamba anakuja vizuri. Lil Ommy hutangaza kipindi cha The Playlist kinachoruka kila Jumamosi saa sita hadi saa nane mchana.

Omary Tambwe aka Lil Ommy

Katika hatua nyingine, Boni Luv alieleza tofauti iliyopo kwenye mchakato wa wasanii kurekodi nyimbo studio, kati ya ilivyo sasa na hali ilivyokuwa miaka hiyo ya 1990.

“Zamani tulikuwa tunarekodia wasanii nyimbo bure kabisa mambo ya wasanii kutoa  pesa ili warekodiwe  yalianza mwaka 1995 na bei  ya kurekodi ilikuwa 5000,  na  hiyo elfu tano  yenyewe bado ilikuwa shida wasanii kuipata,” alisema.

Boni Luv alitunukiwa tuzo ya heshima ya muziki wa kizazi kipya kwenye tuzo za East Africa TV mwaka jana.

Aliyekuwa Waziri wa Habari, Sanaa, Michezo na Utamaduni, Nape Nnauye akimkabidhi tuzo ya heshima DJ Boni Love

Nahodha wa Simba apata ajali, mmoja afariki
JPM amteua Sirro kuwa Mkuu wa Polisi (IGP)