Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mchana wa Alhamis hii limempitisha mheshimiwa Kassim Majaliwa kuwa Waziri Mkuu mpya.

Kuthibitishwa kwa uteuzi wa waziri huo kumefuatia kura za Ndio na Hapana zilizopigwa na wabunge.

Jina lake limepitishwa kwa kura 258 kati ya 351 zilizopigwa sawa na asilimia 73.5. Wabunge 91 walipiga kura za Hapana ambazo ni sawa na asilimia 25.9%.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli alipendekeza jina la Mheshimiwa Majaliwa na kuwasilisha jina lake bungeni.

Akizungumza bungeni humo baada ya kupitishwa na wabunge, Majaliwa alisema hakutegemea kuja kuteuliwa kushika wadhifa huo. Amemshukuru Dkt Magufuli kwa kumwamini na kumteua kushika nafasi hiyo na kuahidi kufanya kazi kwa ufanisi.

“Kwa jukumu nililopewa niwahakikishie wabunge nitashirikiana nanyi kufanya kazi kwaajili ya wananchi waliotupa ridhaa ya kuwawakilisha,” alisema.

Ameahidi pia kufanya ziara katika majimbo yote kuangalia shughuli za maendeleo zinazoendelea huko.

Dk Tulia Akson Mwansasu achaguliwa na kuapishwa kuwa Naibu Spika
Jarida la People lamtaja Beckham kama mwanaume anayevutia zaidi duniani