Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kuwa kina uhakika kuwa kitashinda chaguzi ndogo za ubunge katika majimbo ya Monduli na Ukonga unaofanyika leo, imelezwa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole alisema kuwa utafiti wao unaonesha dhahiri kwa mahesabu kuwa watashinda kwa kishindo katika majimbo hayo.

“Kutokana na takwimu zetu na mafanikio tuliyoyapata wakati wa kampeni zetu katika majimbo yote mawili, tuna uhakika kwa asilimia 100 kuwa tunaenda kushinda,” alisema Polepole.

Aidha, Polepole alitupa lawama kwa vyama vya upinzani kwa madai kuwa walikuwa wakitumia lugha chafu dhidi ya wagombea wao ambao amedai wamehamia CCM kwa sababu zenye mashiko.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Chadema, John Mrema amesema kuwa Makongoro Mahanga aliyekuwa mmoja kati ya wapiga kampeni wake tayari amekwisha omba radhi kwa Tume ya Uchaguzi kwa kutumia lugha isiyofaa kwenye kampeni.

Chadema pia kwa nyakati tofauti wamekuwa wakieleza kuwa wana uhakika wa kushinda katika majimbo hayo mawili, Monduli likiwa linatajwa zaidi kuwa ngome ya Edward Lowassa ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho kikuu cha upinzani.

Yote yatafahamika leo ambapo wananchi wataamua kwenye sanduku  la kura.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amewahakikishia wananchi kuwa ulinzi umeimarishwa katika jimbo la Ukonga, hivyo wajitokeze kwa wingi kupiga kura.

Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Septemba 16, 2018
Mayweather kuzichapa tena na Pacquiao, watambiana uso kwa uso

Comments

comments