Klabu ya Chelsea imekuwa ya pili kujiondoa kwenye dili la kutaka kumsajili kiungo kutoka nchini Ufaransa Paul Pogba, baada ya FC Barcelona kufanya hivyo mwanzoni mwa mwezi huu.

Meneja wa Chelsea Jose Mourinho, ambaye awali alionyesha nia kutaka kufanya kazi na kiungo huyo, amekiri kutokuwa na mpango wowote wa kumsajili Pogba, kutokana na ushindani wa kibiashara uliowekezwa kwa mchezaji huyo.

Mourinho ameweka wazi msimamo wake wa kujiondoa kwenye mbinu za kumsajili Pogba, baada ya kuulizwa na waandishi wa habari huko Amerika ya kaskazini ambapo kikosi chake kimeweka kambi ya kujiandaa na msimu mpya wa ligi.

Amesema ni kama upuuzi kuendelea kumuwania Pogba mwenye umri wa miaka 22, kutokana na baadhi ya watu kutaka kunufaika kimaslahi na kipaji cha kinda huyo aliyepita chini ya utawala wa Sir Alex Ferguson kutokana na ada kubwa ya usajili iliyotangazwa na viongozi wa Juventus.

Mourinho ameendelea kutanabaisha kwamba, kama FC Barcelona walishindwa kumsajili Pogba kwa ada ya uhamisho wa Euro million 80 sawa na paund million 55, anaamini Chelsea haitoweza kabisa kumnasa kiungo huyo kutokana na gharama zake kubwa kubwa.

Kujiondoa kwa Chelsea pamoja na FC Barcelona, kunadhihirisha klabu za Real Madrid, Manchester City pamoja na Paris St Germain zimeachwa katika mchakato wa kumuwania mchezaji huyo ambaye bado ana mkataba na mabingwa wa soka nchini Italia Juventus hadi mwezi June mwaka 2019.

Marekani Yapinga Uhalali Wa Uchaguzi Wa Burundi, Wawili Wauawa
Mario Gomez Aikana Besiktas Ya Uturuki