Chama cha Wananchi (CUF), kimelalamikia kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli kuhusu mkwamo wa kisiasa visiwani Zanzibar kufuatia sintofahamu iliyojitokeza baada ya kufutwa kwa uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka jana  na kufanyika kwa uchaguzi wa marudio ambao chama hicho kiliususia.

Akihutubia katika mkutano wa hadhara uliofanyika Unguja wiki iliyopita, Rais Magufuli alimshauri Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein kutosaini malipo ya matibabu ya Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kufuatia kitendo cha kugoma kumshika mkono hadharani kwenye msiba wa Aboud Jumbe.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Mwenyekiti wa muda wa CUF, Julius Mtatiro alisema kuwa kauli ya Rais Magufuli itaendelea kuleta mgawanyiko visiwani humo na kwamba Maalim Seif hana sababu ya kujipendekeza kwa Dkt. Shein kwani malipo yake yako kikatiba.

“Tunataka kumweleza Rais Magufuli kwamba Dk. Shein hana uwezo wa kumfutia Maalim Seif posho na matibabu kwa sababu hizo ni stahiki zake kikatiba na kisheria,” Mtatiro anakaririwa.

Katika hatua nyingine, Mtatiro alioenesha kusikitishwa na kauli ya Rais Magufuli kutaka Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jecha Salim Jecha kupewa tuzo kwa uamuzi wake wa kufuta matokeo ya uchaguzi wa Oktoba 25 na kuitisha uchaguzi mwingine.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai alisema kuwa kauli ya Rais Magufuli ilikuwa hisia zake juu ya ‘kituko’ alichokifanya Maalim Seif katika msiba ambacho alidai sio cha kiungwana kufanywa na kiongozi huyo.

Salum Mwalimu, Wafuasi Chadema wapata dhamana, ni baada ya Ukuta kuwaweka selo
Biashara na Uwekezaji Wasisitizwa Katika Mkutano wa G20