Mpasuko wa kisiasa visiwani Zanzibar unaotokana na kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 mwaka jana na kufanyika kwa uchaguzi wa marudio umeendelea kuleta mvutano kati ya Serikali inayoongozwa na Rais Ali Shein na Chama Cha Wananchi (CUF).

Akihutubia baraza la Eid jana, Rais Shein aliwataka wapinzani kusahau kuhusu kuundwa kwa serikali ya mpito na kwamba hakuna uchaguzi mwingine utakaofanyika hadi mwaka 2020.

Aidha, Rais Shein aliwaonya wote wanaotaka kukwamisha juhudi za Serikali kutekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

“Nimesikitishwa sana na matukio yote ambayo yamelitia aibu kubwa taifa letu kwani hayaendani na mafunzo tuliyoyapata katika kipindi cha swaumu…tunatakiwa kuacha kujenga kiburi na ufisadi,” alisema Rais Shein.

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amesema kuwa yuko tayari kukamatwa na kufunguliwa mashtaka kwa tuhuma zinazotajwa na Jeshi la Polisi kuwa yeye ndiye anayehamasisha wafuasi wake kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani na kukataa kushirikiana na Serikali.

Maalim Seif ambaye pia alikuwa akihutubia katika baraza la Eid katika ukumbi tofauti na ule ulifoanywa na Rais Shein, alilaani vitendo vinavyofanywa na Jeshi la Polisi akidai kuwa wananchi wananyanyaswa bila kuwa na makosa.

Alisema kuwa endapo watawala wanaona kuwa chanzo cha hayo yote ni yeye, yuko tayari wamkamate ili wasiwasumbue wananchi hao.

“Hakuna haja ya kuwatesa watu, iwapo wanayo azma ya kunikamata, mimi nipo waje tu wanikamate,” alisema Maalim Seif.

Alisema kuwa hali ya maisha ni ngumu na kwamba kwa matendo yanayofanyika visiwani humo ni vigumu kuamini kama Serikali hiyo inaongozwa na Waislamu.

“Mambo hayo yanafanywa kutokana na kushindwa kuzigeuza nyoyo za wananchi ndiyo maana wanafanya hujuma, vitendo vya kikatili na kuwatisha wananchi,” alisema.

Maalim Seif amekuwa akisisitiza kuundwa kwa serikali ya mpito visiwani humo ili kuruhusu kufanyika kwa uchaguzi mwingine utakaosimamiwa na Mamlaka isiyofungamana na upande wowote kati ya CCM na CUF.

BAVICHA wawajibu UVCCM kuhusu mpango wa kwenda Dodoma
Video: Mmarekani Mweusi alivyopigwa risasi sita kifuani na Polisi ‘Mzungu’