Jeshi la Polisi nchini, jana lilizuia kufanyika kwa kongamano lililoandaliwa na Chama cha ACT – Wazalendo kwa lengo la kujadili Bajeti ya Serikali ya mwaka 2016/17 jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Anna Mghwira aliwaambia waandishi wa habari kuwa wamepokea taarifa kutoka kwa vijana wanaofanya maandalizi katika ukumbi uliopangwa kufanyika tukio hilo kuwa Jeshi la Polisi limezuia kufanyika kwa kongamano hilo kwakuwa halina kibali.

“Tumepata taarifa kutoka kwa vijana wetu waliokuwa wanafanya maandizi kuwa uongozi wa jengo tulilopanga kufanyika kongamano umesema umepokea maagizo kutoka polisi kuwa wasiruhusu jambo hilo kwa sababu halina kibali,” alisema Mghwira.

Katika hatua nyingine, Polisi wameripotiwa kumsaka Kiongozi Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe ambaye alipangwa kuwa mzungumzaji mkuu katika kongamano hilo.

Kaimu Katibu Mkuu wa Chama hicho, Msafiri Mtemelwa aliwaambia waandishi wa habari kuwa hawafahamu kiongozi huyo alipo lakini polisi (askari kanzu) wamekuwa wakilinda nyumbani kwake tangu juzi usiku kwa lengo la kumkamata.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Siro na Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Bulimba hawakutoa taarifa yoyote kuhusu tukio hilo japo walitafutwa na waandishi wa habari na kuongea nao kwa njia ya simu. Leo, Jeshi hilo linatarajiwa kutoa taarifa yake rasmi kuhusu matukio hayo.

Baada ya kuikimbia Chadema, Ole Medeye atoa msimamo wake kuhusu Lowassa
Mbowe afungiwa Hotelini, akamatwa na kugomea masharti ya polisi