Wakili Eric Gumbo, anayewakilisha Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) katika ombi linaloendelea la uchaguzi wa urais, amesema kuwa Raila Odinga na mgombea wake Martha Karua hawafai kulaumu tume kwa kushindwa kwa maajenti wao katika vituo vya kupigia kura.

Wakili Gumbo amesema hayo akitoa mawasilisho yake mbele ya sajili ndogo ya Mahakama ya Juu katika Mahakama ya Milimani leo Semptemba 1, 2022.

Wakili Gumbo amesema kuwa makamishna wa IEBC wangeweza tu kutekeleza majukumu mahususi kuhusu mchakato wa kuhakiki kura ambazo ziliunganishwa katika kituo cha kitaifa cha kujumlisha kura.

Wakili Eric Gumbo.

Amesema kuwa itakuwa “haiwezekani” kuwalaumu makamishna kwa kile ambacho wakala alipaswa kufanya katika vituo vya kuhesabia kura za majimbo na kaunti, ili kuhakikisha maingizo yanayofaa yameingizwa katika Fomu 34A.

“Itakuwa si sahihi na haitawezekana kutarajia makamishna hao saba ndio watafanya kazi zote mahususi ambazo tume ilipaswa kufanya,” amesema Gumbo. 

Aidha amewafananisha mawakala na wanandoa akisema chama kinaruhusiwa kujichagulia mawakala wao na iwapo watashindwa kuelewa wajibu wao wanapaswa kulaumiwa kwa makosa yoyote na si tume.

“Mawakala ni kama wenzi wetu unachagua wako na unayemwamini. Hakuna mtu anayeweka wakala kwako, ukichagua mmoja huna imani naye huwezi kumlaumu mtu yeyote,” aliongeza.

Pia Gumbo amebainisha kuwa ni jukumu la wakala kuthibitisha madai katika maeneo ambayo kuna makosa wakati wa uchaguzi yalishuhudiwa na sio “kulemea mahakama” bila uthibitisho wa kutosha. 

“Tunapotoa tuhuma hizi katika maombi yetu ya uchaguzi, pengine tunatakiwa kujiuliza kama tumefanya yale ambayo sheria inatuelekeza na kwamba iwapo sheria itakupa fursa ya kuchagua wakala wako ili kukuthibitishia kuhusiana na mchakato wa uchaguzi,” amesema Gumbo.

 

Serikali 'yatangaza vita' na wauzaji ardhi kiholela
Kizungumkuti upatikanaji wa 'saver' IEBC