Timu ya taifa ya Tanzania bara (Kilimanjaro Stars) imepoteza mchezo watatu mfululizo wa hatua ya makundi, kwenye michuano ya kombe la Challenge inayoendelea nchini Kenya na kuondolewa rasmi kwenye michuano hiyo.

Kilimanjaro Stars imemaliza hatua ya makundi kwa kufungwa na Kenya bao moja kwa sifuri, na kujikuta ikiburuza mkia wa kundi A, ambalo linaongozwa na wenyeji Harambee Stars wakifuatiwa na Zanzibar, Libya, na kisha Rwanda.

Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Alex Muhabi aliyesaidiwa na Dick Okello na Ronald Katenya, wote wa Uganda, bao pekee la Harambee Stars lilifungwa na Vincent Ouma dakika ya 19, akimalizia mpira uliotemwa na kipa Peter Manyika baada ya krosi ya Ochieng Ovella aliyempita kutoka kwa chenga ya hadi chenga beki Kennedy Wilson.

Kilimanjaro Stars ilianza kwa kupeleka mashambulizi langoni mwa Harambee kusaka bao la kusawazisha, lakini hawakufanikiwa. Kenya wanafikisha pointi nane na kumaliza juu ya kundi wakifuatiwa na Zanzibar waliomaliza na pointi saba.

Mchezo mwingine wa Kundi A uliotangulia mchana wa leo, Libya ilishinda 1-0 dhidi ya Zanzibar, bao pekee la Alharaish Zakaria dakika ya 24 Uwanja wa Jomo Kenyatta mjini Machakos, Kenya leo, wakati mchezo wa mwisho wa Kundi B, Burundi iligawana pointi na Sudan Kusini baada ya sare ya 0-0 Uwanja wa Bukhungu mjini Kakamega.

Hiyo inamaanisha Uganda inamaliza kileleni mwa Kundi B kwa pointi zake tano sawa na washindi wa pili, Burundi ambao wanazidiwa wastani wa mabao.

Kwa mantiki hiyo Zanzibar itakutana na mabingwa watetezi, Uganda katika mchezo wa Nusu Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, Desemba 15, mwaka huu.

Hiyo itakuwa Nusu Fainali ya pili, baada ya Nusu Fainali ya kwanza kati ya wenyeji, Kenya dhidi ya Burundi Desemba 14.

Magazeti ya Tanzania leo Desemba 12, 2017
West Ham Utd wamshtua Antonio Conte