Kiongozi wa Kanisa Katoliki nchini Zimbabwe anatarajia kuongoza kikao maalum kati ya Rais Robert Mugabe na Mkuu wa Majeshi ya nchi hiyo kuzungumzia sintofahamu ya madaraka iliyoibuka tangu Jumatano iliyopita.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotangazwa na kituo cha runinga cha Taifa hilo, Mugabe na Mkuu wa Majeshi watafanya kikao kutafuta muafaka huku maelfu ya watu wakiendelea na maandamano makubwa ya kumtaka aachie madaraka.

Katika hatua nyingine, chama tawala cha Zanu-PF ambacho kwa sasa kina mpasuko kimepanga kufanya mkutano wake kujadili hatma ya uongozi wa Mugabe.

Jeshi liliingilia mgogoro wa madaraka ndani ya nchi hiyo baada ya Rais Mugabe kumfuta kazi aliyekuwa Makamu wake wa Rais, Emmerson Mnangagwa ambaye anatajwa kuwa kati ya wapigania uhuru wa nchi hiyo.

Kutokana na hatua hiyo, Mke wa Mugabe, Grace Mugabe alitajwa kuwa na nafasi kubwa zaidi ya kurithi madaraka ya Mumewe.

Hata hivyo, Mugabe amekuwa akisisitiza kuwa angegombea tena katika uchaguzi wa Rais unaokuja.

Jeshi limeendelea kusisitiza kuwa hatua yao sio kuipundua serikali ya Mugabe bali ni kuwaondoa wahalifu wanaomzunguka.

Rais Mugabe alionekana kwa mara ya kwanza hadharani kwenye mahafali ya Chuo Kikuu Huria cha Zimbabwe jijini Harare akiwa ndiye Mkuu wa Chuo hicho, tangu hatua ya Jeshi kuingilia mgogoro huo.

Watendaji wa Serikali watakiwa kuzingatia mwongozo wa Bajeti
Magazeti ya Tanzania leo Novemba 19, 2017