Polisi wa kutuliza ghasia nchini Kenya, wametumia mabomu ya machozi kuwatawanya waandamanaji waliokusanyika jijini Nairobi kushiriki maandamano yaliyoitishwa na upinzani, kupinga upandaji wa gharama ya maisha.
Hatua hiyo inafuatia kiapo cha Serikali ya Rais William Ruto, kuwa na misimamo mikali kuhusu maandamano hayo ambayo kinara wa upinzani Raila Odinga naye aliapa kuwa yataendelezwa licha ya kutopokea kibali cha polisi.
Waandamanaji hao, pia waliwarushia mawe polisi wa kupambana na ghasia nje ya ofisi za serikali katika mji mkuu, huku takriban watu 22 wakikamatwa, wakiwemo wabunge wawili na biashara nyingi zilifungwa, huku wafanyakazi wengi wakisalia majumbani.
Odinga, aliwaambia wafuasi wake wajitokeze na waonyeshe kutofurahishwa na kinachotokea nchini mwao, akidai Wakenya wanateseka kutokana na kupanda kwa bei ya mahitaji ya kimsingi, kushuka kwa kasi kwa shilingi ya ndani dhidi ya dola ya Marekani, na ukame ambao umesababisha njaa kwa mamilioni.
Mmoja wa waandamanaji, Charles Oduor (21), amesema, “tulikuja hapa kwa amani lakini walitupiga mabomu ya machozi, wanatudanganya kila siku uko wapi unga wa bei nafuu wa mahindi walioahidi? Kazi ziko wapi kwa vijana walioahidi? Wanachofanya ni kuajiri marafiki zao tu.”
Hata hivyo, Mkuu wa polisi wa Nairobi, Adamson Bungei alisema Polisi walipokea maombi ya kufanya maandamano mawili mwishoni mwa Jumamosi na mapema Jumapili (Machi 18 na 19, 2023), kinyume na notisi ya kawaida ya siku tatu inayohitajika kwa mikutano ya hadhara.
Aidha, naye Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya, Kithure Kindiki alionya kuwa mtu yeyote anayechochea ghasia za umma au kuvuruga amani atachukuliwa hatua, licha ya Odinga kusema aliitisha maandamano kupinga upandaji wa gharama ya maisha na uchaguzi ulioibiwa Agosti mwaka jana (2022).