Mshambuliaji kutoka Tanzania Elias Maguri, amesema ni heshima kwake kuwa sehemu ya kikosi cha FC Platinum kilichowasili nchini mwishoni mwa juma lililopita, tayari kwa mchezo wa mkondo wa pili wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Simba SC.

Mshambuliaji huyo ambaye aliwahi kuitumikia Simba SC, hakuwa sehemu ya kikosi kilichocheza dhidi ya Simba SC katika mchezo wa mkondo wa kwanza mjini Harare, Zimbabwe Desemba 23, 2020.

Maguri amesema suala la kuwa kwenye msafara wa FC Platinum uliowasili jijini Dar es salaam Jumamosi (Januari 02), ni jambo la heshima na farahi kwake, hata kama hatokua sehemu ya kikosi kitakachoanza siku hiyo.

“Ni jambo kubwa lakini la heshima kwangu na timu yangu kwa sababu sikuweza kuwepo katika mchezo wa kwanza kutokana na majeraha niliyoyapata siku nne kabla ya mchezo.”

Kuhusu mipango ya kuelekea mchezo wa mkondo wa pili utakaochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa Jumatano (Januari 06), Maguri amesema wamekuja nchini kupambana ili kutimiza lengo la kutinga kwenye hatua ya makundi ya michuano hiyo ya Afrika.

“Mchezo wa marudiano naamini utakuwa mgumu japo ushindi kwetu ni kitu muhimu, lengo letu ni kusonga mbele kwenye hatua ya makundi, ninaamini tutafanikiwa.” amesema Maguri.

Katika mchezo wa Janauri 06, Simba SC itatakiwa kushinda mabao mawili kwa sifuri na kuendelea ili kujihakikishia safari ya kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu huu, huku FC Platnum wakihitaji sare ama ushindi kufikia lengo la kuwatupa nje Mabingwa hao wa Tanzania Bara.

Young Africans yaweka mguu sawa Mapinduzi CUP
Azam FC yawakana Chikwende, Mgore