Jaji mwandamizi nchini Nigeria, James Agbadu-Fshim, amesimamishwa kazi kwa tuhuma za kupokea rushwa kutoka kwa wanasheria waliokuwa na kesi mbalimbali mahakamani.

Upelelezi wa awali umeonesha kuwa jaji huyo alipokea fedha kupitia akaunti zake za benki kutoka kwa watu ambao walibainika kuwa ni wanasheria aliokuwa anasikiliza kesi zao mahakamani.

Taarifa ya Baraza la Taifa la Mahakama iliyotolewa jana imeeleza kuwa katika utetezi wake, Jaji Fishim alidai kuwa alipokea fedha hizo kama msaada kutoka kwa rafiki zake kutokana na kucheleweshwa kwa mshahara wake.

Jaji huyo husikiliza kesi katika mahakama ya Taifa ya Viwanda na sasa amesimamishwa huku Baraza la Mahakama likiandika mapendekezo kwa Rais ili aondolewe.

Tuhuma kama hizo za rushwa pia zimemuendea jaji Rita Ajumogobia baada ya kubainika kuwa wafanyakazi wa serikali pamoja na watu wengine wamekuwa wakiweka fedha kwenye akaunti zake za Benki.

Majaji wote wawili walisimamishwa jana wakisubiri hatma yao baada ya Rais Muhammadu Buhari kutoa majibu ya mapendekezo ya Baraza la Mahakama.

Tangu alipoingia madarakani mwaka 2015, Rais Buhari aliahidi kupambana na rushwa na ufisadi uliokuwa umekithiri.

Ripoti ya kupima viwango vya rushwa ya ‘Transparency International’s Corruption Perceptions Index’ ya mwaka 2017, imeiweka Nigeria katika nafasi ya 27 kwa nchi zenye rushwa zaidi duniani.

Video: Ali Kiba aachia ‘Mwambie Sina’ akiwa na wasanii wake
Mhadhiri UDOM anaswa 'akijaribu kupokea' rushwa ya ngono