KOCHA Msaidizi wa timu ya Azam FC, Mario Marinica raia wa Romania, amesema kuwa wana kikosi bora kabisa hivi sasa, kinachoweza kuifunga timu yoyote ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

Marinica ametoa kauli hiyo ikiwa ni siku nne tu zimebakia kabla ya Azam FC kuvaana na Simba kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa ligi unaosubiriwa kwa hamu na mashabiki wengi wa soka nchini.

Mromania huyo ameuambia mtandao wa azamfc.co.tz, kuwa kila mchezaji wao aliyekuwa kikosini ni bora na ndio maana amepata nafasi ya kusajiliwa na Azam FC.

“Tuna uhakika tutashinda dhidi ya Simba, licha ya kuwa na muda mdogo wa kufanya maandalizi kutokana na wachezaji wetu wengi kuwa nje ya timu kwa muda mrefu wakiwa kwenye majukumu ya timu za Taifa,” alisema.

Alisema wanakabiliana na changamoto mbalimbali za baadhi ya wachezaji wao waliorejea kutoka timu za Taifa kuwa na majeraha madogo.

Aliongeza kuwa: “Viongozi wa soka la Tanzania walipaswa kuziongezea muda wa maandalizi timu zilizokuwa na wachezaji kwenye timu za Taifa. Tena ukizingatia mechi inayokuja ni kubwa sana (derby), ili kupata kiwango kikubwa kulingana na mechi yenyewe, lazima upate muda wa kujiandaa. Huwezi kutegemea mchezo mzuri kwa aina ya maandalizi haya ya haraka haraka.”

Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, amesema leo kuwa amezitumia siku mbili za mazoezi ya jana na leo kuwarudisha wachezaji wake kwenye staili ya uchezaji ya Azam FC baada ya kutoka timu za Taifa.

“Nadhani Baada ya kuwakusanya wachezaji pamoja waliotoka timu za Taifa, jambo la kwanza linakuwa ni kuwafanya wafurahi na kuifikiria Azam FC tu kwa sababu wanaporejea kambini huwa wanafikiria Taifa Stars, Zanzibar Heroes, Kenya, Burundi ambako wametoka na sio Azam.

“Kwa hiyo jana na leo, jambo kubwa tulilokuwa tunafanya tumejaribu kuwafanya wachezaji wasahau mambo ya timu ya Taifa na kujua ya kuwa kwa sasa wapo Azam FC na wana mchezo muhimu Jumamosi dhidi ya Simba,” alisema.

Alisema kuwa baada ya hapo wataanza kufanya tathimini ya wachezaji majeruhi na kasha kuanza kutoa mbinu kuelekea mchezo huo.

Akizungumzia kutoripoti kwa kiungo wake, Jean Baptiste Mugiraneza ‘Migi’, alisema kuwa: “Mugiraneza bado yupo Addis Ababa baada ya kumaliza majukumu yake na timu ya Taifa ya Rwanda, anafanya nini Ethiopia wakati michuano imeisha tokea Jumamosi.

“Hii imetushushia heshima sisi, anatakiwa kuwa hapa hivi sasa na kufanya mazoezi na sisi, tunamlipa mshahara na sio Rwanda wala Cecafa inayofanya hivyo. Cecafa haijafanya jambo zuri kwenye hili.”

Wachezaji wa Azam FC waliokuwa kwenye michuano ya Chalenji, ambao mpaka sasa wamesharipoti ni nahodha John Bocco ‘Adebayor’, nahodha msaidizi Himid Mao ‘Ninja’, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Ame Ally ‘Zungu’, Shomari Kapombe, Aishi Manula.

Wengine ni Didier Kavumbagu, Allan Wanga, Khamis Mcha ‘Vialli’, Mwadini Ally, Mudathir Yahya, ambao wameungana na wenzao walioanza mazoezi wiki mbili zilizopita na kupata fursa ya kufanya ziara ya siku tano Tanga, iliyomalizika juzi.

Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB, ndio vinara wa ligi hivi sasa wakiwa na pointi 25 baada ya kushinda mechi nane na sare mchezo mmoja, waliocheza na Yanga wanaokamata nafasi ya pili kwa pointi 23.

Kikosi Cha Vijana (U15) Charejea Dar es salaam
Nahodha Wa Yanga Nadir Haroub Atangaza Kustaafu Soka