Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ameteua timu mpya ya wataalamu saba kwa ajili ya kusimamia mradi wa ujenzi wa jengo la tatu la abiria (Terminal III), katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere.

Hatua hiyo imefikiwa kufuatia agizo la Rais Dkt. John Magufuli alilolitoa jana wakati alipofanya ziara ya kushtukiza uwanjani hapo  kujionea maendeleo yaliyofikiwa katika mradi huo.

Timu hiyo inaongozwa na Eng. Julius Ndyamukama, Eng, Godson Ngomuo, Eng. Humphrey Kanyenye, Eng. Abednego Lyanga, Eng. Mbila Mdemu na Eng. Rehema Myeya.

“Naamini timu hii ina wataalamu mahiri, hivyo itasimamia ujenzi huu kukamilika kwa wakati na kwa kuzingatia thamani ya fedha (value for money”, amesema Mbarawa.

Aidha, ameitaka timu hiyo kuhakikisha ujenzi wa jengo hilo unakamilika mwezi Desemba mwaka huu kama ilivyopangwa.

Kwa upande wake Meneja wa mradi huo Eng. Julius Ndyamukama, ameahidi kushirikiana na wenzake katika kuhakikisha mradi huo unamalizika kwa wakati.

Katika hatua nyingine Profesa Mbarawa amemsimamisha kazi Meneja wa Fedha kutoka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini (TAA), Simba Lugando kwa kuidhinisha malipo ya ujenzi wa Uwanja wa ndege wa Songwe mkoani Mbeya kwa mkandarasi wa Kampuni ya DB Shapriea kiasi cha shilingi Bilioni 3.3 ambapo ujenzi wake haukufanyika ipasavyo.

 

Viongozi wa dini wamuunga mkono Makonda kuhusu dawa za kulevya
Video: Askofu Gwajima ajibu tuhuma madawa ya kulevya