Mshambuliaji wa pembeni kutoka nchini Tanzania na klabu ya Wydad Casablanca ya Morocco, Simon Msuva ametangaza njaa ya kusaka tuzo ya ufungaji bora kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, msimu huu 2020/21.

Msuva ametangaza njaa ya kusaka mabao kwenye michuano hiyo, kufuatia kuwa na mwanzo mzuri akiwa na klabu yake ya Wydad Casablanca iliyopangwa kwenye Kundi C, na tayari imeshacheza michezo minne.

Mshambuliaji huyo ambaye aliifungia Taifa Stars bao la ushindi dhidi ya Libya mwishoni mwa juma lililopita, tayari ameshafunga mabao mawili kwenye michuano hiyo, na amesisitiza kuwa na matumaini ya kuendelea kufunga zaidi kwenye michuano hiyo.

“Mimi kwa sasa nina magoli mawili, anayeongoza ana mabao matatu, kwa hiyo utaona bado nina nafasi nzuri tu ya kuwa mfungaji bora na hilo ndilo lengo langu,” amesema Msuva.

Mbali na ufungaji bora, Msuva amesema anataka kuipa timu yake ya Wydad ubingwa wa Afrika ambapo ndiyo malengo makubwa yaliyowekwa na viongozi wao wa juu kwa msimu huu.

Timu hiyo anayoichezea Msuva, tayari imeshafanikiwa kutinga hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ikiwa inaongoza kwenye Kundi C kwa kufikisha alama 10.

Mchezaji anayeongoza kwa ufungaji mabao mpaka sasa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ni Ayoub El Kaabi ya Wydad ya Morocco akiwa na mabao matatu, huku Msuva wa timu hiyo hiyo, Luis Miquissone na Chris Mugalu wote wa Simba SC wakiwa na mabao mawili kila mmoja.

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Aprili 2, 2021
UEFA wafanya mabadiliko EURO 2020