Takriban watu 10 wameuwawa, baada ya mapigano mapya kuzuka kati ya wakulima na wafugaji eneo la kusini mwa Taifa la Chad.
Taarifa ya Gavana wa Mkoa wa Madoul, Adoum Forteye imeeleza kuwa mtoto mmoja wa kiume mwenye miaka 12 kutoka jamii ya wafugaji aliwapeleka wanyama na kuwalisha katika shamba la mkulima wa karanga hali iliyoibua ugomvi uliosababisha kifo cha kijana huyo.
Amesema, katika hatua ya kulipa kisasi wazazi wa kijana huyo waliwauwa wakulima tisa katika kijiji cha Bara II kilomita 600 kusini mashariki mwa mji mkuu N’Djamena ambapo wafugaji watano na mtu anayetuhumiwa kumuuwa mtoto huyo wamekamatwa.
Wakulima katika eneo hilo, wamekuwa wakiwatuhumu wafugaji kwa kulisha mifugo mazao yao na kuyaharibu, huku wafugaji wakisema wana haki ya asili ya kuilisha mifugo kwenye maeneo hayo hali inayosababisha machafuko maeneo yenye rutuba ya mpakani mwa Chad, Kameruni na Jamhuri ya Afrika ya kati.