Siku chache baada ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kudaiwa kuzuia uendeshaji wa runinga za mtandaoni (online TV), Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye ametengua zuio hilo.

Nnape ameeleza kuwa ameamua kusimamisha zuio hilo kwakuwa halitakuwa na tija kwa wakati huu kwani kanuni zinazotoa muongozo wa namna ya kuendesha maudhui ya mtandaoni bado ziko kwenye mchakato na hazijakamilika.

“Mpaka tutakapokamilisha kanuni ndipo tutakapokaa na wadau tuzungumze namna ya kuendesha hizo ‘online content’ zote. Serikali inafanya mchakato huo, tuko katika hatua za mwisho. Zitakapokamilika tutawaita wadau,” Nnape ameiambia Clouds FM.

“Hakuna sababu ya kuharakisha kwenda kuwafungia watu bila kuwa na sheria au kanuni ambazo zinalielezea jambo lenyewe,” aliongeza.

Waziri huyo alifafanua kuwa ni lazima uendeshaji wa maudhui ya mitandaoni kwa wana habari ifuate kanuni na sheria na kwamba kanuni zinazokuja hazitakuwa na nia ya kuzuia bali kusimamia (regulate).

Alisema nia ya kuweka kanuni hizo ni kuhakikisha kunakuwa na uwajibikaji wa watumiaji wa maudhui ya mtandaoni na wanaoweka maudhui hayo na kwamba utaratibu huu hufanyika kote duniani.

Hivi karibuni, zilisambaa picha za baadhi ya wanahabari wanaoendesha runinga za mitandaoni wakiwa na maafisa wa TCRA na ikaelezwa kuwa wametakiwa kusitisha kazi hiyo hadi maelekezo zaidi yatakapotolewa.

Video: JPM achukizwa mzaha vita dawa za kulevya, Gwajima afunguka...
Elimu yazidi kuporomoka visiwani Zanzibar