Waziri wa Habari, Utamaduni, Michezo na Wasanii, Nape Nnauye amewashukia watendaji wa Shirika la Habari nchini (TBC) baada kurusha moja kwa moja harusi kwa muda wa masaa mawili hali iliyozua maswali mengi kwa wananchi kwa kuwa shirika hilo hutumia fedha za umma.

Jana, Nape aliwaagiza watendaji wa TBC kutoa maelezo ya kina kuhusu uamuzi wa kurusha moja kwa moja matangazo hayo ya harusi.

TBC1 juzi ilirusha moja kwa moja matangazo ya Harusi kutoka ukumbini hali ambayo ni tofauti kwani wana kipindi kilichorekodiwa na kuhaririwa cha ‘Chereko’. Baadhi ya matukio yaliyokuwa kwenye harusi hiyo iliyorushwa moja kwa moja pamoja na urefu wa muda, vilionekana kutowafurahisha baadhi ya watu na kuanzisha gumzo kwenye mitandao ya kijamii.

“Mimi pia nilikiona kipindi hicho na nimepata malalamiko mengi ya wadau na wananchi juu ya tukio hilo. Naamini limeudhi wengi. Nimeagiza niletewe maelezo ya kina kabla ya kuona hatua za kuchukua kulinda heshima ya Televisheni ya Taifa,” alisema Nape.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Clement Mshana alisema kuwa kipindi hicho kilikuwa sehemu ya kipindi cha Chereko na kwamba kwa kuwa ilikuwa wikendi, ni ruksa  mtu kulipia muda wa kurusha moja kwa moja harusi yake kama sehemu ya tukio hilo.

Madiwani wa CUF Kufikishwa Mahakamani Kwa Kufanya Vurugu
Video Mpya: Ommy Dimpoz - Achia Body