Mshambuliaji wa klabu ya Young Africans Ditram Nchimbi amekosekana katika mazoezi ya timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ yanayofanyika leo asubuhi, Uwanja wa Benjamini Mkapa.

Awali katika mazoezi ya jana Jumanne (Machi 9) mshambuliaji huyo hakuwa sehemu ya wachezaji waliokua uwanjani wakiendelea na mazoezi, na badala yake alikuwa amekaa pembeni pembeni akiwafuatilia wachezaji wenzake.

Kocha Mkuu wa ‘Taifa Stars’ Kim Poulsen pamoja na daktari wa timu  Richard Yomba walikuwa wakizungumza na kumuita mchezaji huyo ambaye alipofika karibu yao alionyesha sehemu ya msuli wake wa paja.

Katika mazoezi ya leo Jumatano (Machi 10) asubuhi mshambuliaji huyo ambaye ana ukame wa kufunga mabao kwa muda wa mwaka mmoja akiwana Young Africans, hakuonekana kabisa hata kuangalia mazoezi kama ilivyokuwa jana jioni.

Mtu wa karibu na mchezaji huyo amesema, Nchimbi baada ya kuonekana hali yake inahitaji kupumzika wamemuondoa kikosini kabisa.

“Jana mbona baada ya kutoka mazoezini alienda kambini kwao akachukua vifaa akarudi nyumbani, hayupo tena na timu.” Amesema mtu huyo.

Taifa Stars inajiandaa kucheza michezo miwili ya kirafiki dhidi ya Kenya Machi 15 na Machi 18  kisha itaenda kucheza michezo kuwania kufuzu AFCON dhidi ya Equatorial Guinea, Machi 25.

Msafara wa Makamu wa pili wa Rais Zanzibar wapata ajali
Namungo FC kuitunishia msuli Raja Casablanca leo?