Beki na nahodha wa klabu ya Manchester City, Vincent Kompany ataendelea kuwa nje ya uwanja kwa kipindi kingine cha miezi mitatu ijayo.

Meneja wa klabu hiyo ya Etihad Stadium, Manuel Pellegrini amethibitisha taarifa za kuendelea kukosekana kwa beki huyo kutoka nchini Ubelgiji, alipozungumza na vyombo vya habari kuelekea mchezo wa hii leo wa ligi ya nchini England ambapo matajiri hao wa mjini Manchester watapapatuana na Everton.

Pellegrini, amesema Kompany, bado anaendelea kupatiwa matibabu na haitokua rahisi kwa sasa kurejea kikosini mwake, kutokana na ushauri ambao amekua akiupokea kutoka kwa madaktari wa klabu ya Man City.

Meneja huyo kutoka nchini Chile amedai kwamba, kutokuwepo kwa beki huyo mwenye umri wa miaka 29 ni pigo kubwa sana kwake, lakini hana budi kukubaliana na hali halisi huku akiwaamini wachezaji waliosalia kikosini kwa sasa.

Hata hivyo Pellegrini, hakuweka wazi tarehe maalum ambayo inadhaniwa huenda ikawa sahihi kwa Kompany kurejea uwanjani zaidi ya kusisitiza huenda akawa fit katika michezo ya mwisho ya msimu huu wa ligi.

Kompany, kwa mara ya mwisho alionekana kikosini wakati wa mchezo wa ligi dhidi ya Sunderland, disemba 26 mwaka 2015, ambapo Man city walichomoza na ushindi wa mabao manne kwa moja.

Katika mchezo huo Kompany hakurejea uwanjani wakati wa kipindi cha pili, kutokana na maumivu makali ambayo yalikua yakimsumbua katika kiazi cha mguu.

Manchester City's Vincent Kompany goes off injured

Tayari Kompany ameshaeleza masikitiko ya kukosekana kwake kupitia kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook, kwa kueleza inamuumiza kuona bado anahitajika kikosini katika kipindi hiki kigumu cha ushindani, lakini inamuuwia vigumu kutokana na hali ya majeraha inayomsumbua.

Man City imekua ikinufaika na uwepo wa Kompany kutokana na rekodi yake kuwa nzuri katika safu ya ulinzi, na mara kadhaa anapokua nje ya uwanja wamekua wakikubali kufungwa kirahisi.

Mkwasa Awapa Dozi Ya Siku 1 Makocha Zanzibar
Samatta Azawadiwa Kiwanja Na Fedha