Aliyewahi kuwa mwenyekiti wa klabu ya Simba SC Alhaji Ismail Aden Rage amesema  ana matumaini ya kuiona klabu hiyo ikitinga hatua ya nusu fainali kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, licha ya kufungwa mabao manne kwa sifuri dhidi ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.

Simba SC ilipoteza kwa idadi hiyo ya mabao ikiwa ugenini FNB Stadium (Soccer City) Afrika Kusini Jumamosi (Mei 15) katika mchezo wa mkondo wa kwanza, na mwishoni mwa juma hili itacheza nyumbani jijini Dar es salaam katika uwanja wa Benjamin Mkapa kwenye mchezo wa mkondo wa pili.

Rage amesema hakuna linaloshindikana katika soka, huku akikumbushia klabu yake ya Simba iliwahi kufanya maajabu mwaka 1979 kwa kuifunga Mufulila Wanderers mabao matano kwa sifuri, baada ya kufungwa nyumbani mabao manne kwa sifuri na timu hiyo kutoka Zambia.

“Hakuna linaloshindikana katika mpira, Simba iliwahi kuishangaza Afrika hapa mwaka 1979, jambo la msingi wachezaji wanatakiwa kupambana na kuondoa fikra za kufungwa mabao manne katika mchezo wa mkoano wa kwanza, kama watafanya hivyo tutafanikiwa,”

“Binafsi ninaiamini sana timu yangu, kwa sababu msimu huu imeonesha kupambana katika michuano hii ya Afrika, hivyo sina shaka na hilo jambo, benchi la ufundi litabuni mbinu mpya ambazo zitawafanya wachezaji kutambua makosa yao na kupambana kwa njia mbadala dhidiya Kaizer Chiefs hapa nyumbani Tanzania.” Amesema Rage.

Kufuatia kufungwa mabao manne kwa sifuri ugenini, Simba SC itatakiwa kushinda mabao matano kwa sifuri, ili itinge hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.

Kipigo cha Simba SC chamgusa Masau Bwire
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Mei 17, 2021