Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Samia Hassan Suluhu amewataka wanachama wa bonde la mto Nile (NBI) kuongeza ushirikiano na kuanzisha programu za maendeleo ili kuwa na matumizi sahihi ya maji ya bonde la mto huo.

Samia ameyasema hayo wakati akizungumza katika maadhimisho YA 18 ya siku ya Nile (Nile day) yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam hivi karibuni.

“Ningependa kuona kuna programu mbalimbali zinawekwa ili kupata picha halisi ya wapi tunaelekea kwa sababu watu milioni 350 wapo katika Bonde la Mto Nile na wanalitumia kwa ajili ya Maji,Nishati na Chakula,kwahiyo ni lazima kuwepo na programu zitakazosaidia kuhifadhi mazingira ya bonde hili”,amesema Samia

Aidha, amesema kuwa kipengele muhimu katika kufanikisha suala la kulinda mazingira ya mto Nile ni  kwa wanachama kukaa pamoja na kuweka sawa masuala ya usimamizi wa maji, matumizi mazuri ya rasilimali zilizopo, utawala bora, ukuaji wa idadi ya watu na mabadiliko ya hali ya hewa katika eneo hilo la bonde la mto Nile.

Pia ametoa wito kwa Sekta binafsi na washirika wa maendeleo kushiriki kwa karibu katika suala hili na hasa watu wa utafiti kufanya utafiti wa kisayansi katika kupata majibu ya masuala mbalimbali yanayojitokeza katika Bonde hilo.

Kwa upande wake, Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge amesema kuwa maadhimisho hayo ya siku ya Nile yana lengo kuu la kujenga uelewa kwa jamii na nchi wanachama juu ya umuhimu wa kulinda vyanzo vya maji yanayopeleka katika mto Nile na hivyo kuyalinda kwa hali na mali kwani eneo hilo lina idadi ya watu 350 milioni na hivyo ushirikiano zaidi unahitajika kulinda mazingira yake.

Katika maadhimisho hayo ya 18 ya Bonde la mto Nile pia mawaziri mbalimbali kutoka nchi kumi(10) wanachama wamesisitiza katika kulinda mazingira, usalama, ushirikiano bora, kulinda mazingira ya bonde hilo, kuzuia mmomonyoko wa ardhi  na ulinzi wa vyanzo vya maji ya mto Nile

Mrema amshukia tundu Lissu kuhusu watuhumiwa wa dawa za kulevya
Makamba apiga marufuku shughuli za kilimo na uchimbaji bonde la msimbazi