Jeshi la ulinzi wa taifa na mashirika ya kiusalama nchini, yametakiwa kuwasaka na kuwakamata maafisa wa Polisi wasio waaminifu, ambao wamekuwa wakishirikiana na wananchi kuharibu miundombinu ya mradi wa reli ya kisasa ya SGR.
Wito huo umetolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango wakati akizindua ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), Tabora – Isaka yenye urefu wa kilomita 165 Mkoani Shinyanga.
Hata hivyo, Dkt Mpango amesema waharibifu hao ni pamoja na madereva na waendeshaji wa mashine kwenye mradi huo, watu wanaoishi karibu na maeneo ya mradi na Maafisa wa Polisi wasio waaminifu wanaolinda mradi huo.
Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya Habari, hadi kufikia sasa Polisi tayari imeshawakamata watu kadhaa wanaohusishwa na uharibifu wa miundo mbinu ya mradi huo wa SGR, ikiwemo kuiba mafuta, saruji na vyuma.