Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Stergomena Tax ametoa wito kwa Taasisi mbalimbali nchini kuendelea kutunza kumbukumbu za historia ya Tanzania na mchango wake katika medani za kikanda na kimataifa ili kuvirithisha vizazi vya sasa na vijavyo.
Kauli hiyo ameitoa jijini Dodoma hivi karibuni wakati wa hafla kukabidhi Machapisho ya
Hashim Mbita kwa Taasisi 18 ambapo alisema Tanzania ina historia nzuri katika medani za kikanda na kimataifa ikiwemo mchango wake katika harakati za ukombozi kusini mwa Afrika.
Amesema, “Wizara imeamua kuyakabidhi machapisho hayo kwa Taasisi hizo ili yasaidie kurithisha
historia iliyomo kwa vizazi vijavyo, na kujenga hamasa ya uzalendo kwa vizazi vya sasa na vijavyo na
inawakabidhi machapisho haya kama wawakilishi wa wengi.”
Kupitia machapisho hayo, historia kuhusu mchango uliotolewa na Tanzania katika harakati za ukombozi wa Kusini mwa Afrika na Afrika kwa ujumla itatunzwa na kukumbukwa huku Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akisema kwamba, Wizara imepokea makasha 28 ya Chapisho la Hashim Mbita.