Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa amesema Serikali inawathamini wazalishaji wa Chumvi hapa nchini, itahakikisha inaondoa changamoto zote zinazokwamisha maendeleo katika Sekta ya Madini, ili uchimbaji wa madini ufanyike kwa tija.
Dkt. Kiruswa, ameyasema hayo Februari 18, 2023 wakati alipotembelea machimbo ya chumvi ya Chakulu Wilayani Uvinza – Kigoma na kuzungumza na kikundi cha Kinyo Farmers and Salt Works na Kikundi cha Twikome Salt Kinyo Chakulu.
Amesema, “Ninasisitiza kuondoa migogoro katika eneo hili ili kuchochea ongezeko la uzalishaji wa Chumvi hapa nchini ili wachimbaji wanufaike na rasilimali hii muhimu.”
Katika hatua nyingine, Dkt Kiruswa amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Uvinza kwa Kushirikiana na Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kigoma, wafanye kikao na Wamiliki wa leseni na Àrdhi siku ya Jumatatu tarehe 20/02/2023, kwa ajili ya kuandika makubaliano ya mkataba.
Aidha, ameiagiza Tume ya Madini kushirikiana na Taasisi ya Jiolijia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), kutembelea maeneo ya leseni za vikundi vyote ili kubainisha maeneo ambayo yanaweza kuchimbwa visima vya kuzalishia Chumvi.
Kwa upande wake, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kigoma, Mhandisi Pius Lobe amevitaka vikundi hivyo wakubaliane ili kuondoa migogoro waliyonayo. Aidha amewataka kufuata maelekezo yaliyotolewa na Dkt. Kiruswa ili kuendelea na uzalishaji.
Hata hivyo, Meneja wa Leseni wa Tume ya Madini, Samwel Mayuki amewataka wamiliki wa leseni na wamiliki wa ardhi kukubaliana na pendekezo la kuingia makubaliano ili kuepuka kusitishwa kwa shughuli za uzalishaji wa chumvi endapo mgogoro huo utaendelea au kutakiwa kufanyika kwa fidia ya ardhi.
Naye, Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kusini, Nashoni Bidyanguze amemshukuru Dkt. Kiruswa kwa kufika kutatua mgogoro huo wa chumvi ambao umechukua muda mrefu. Amesisitiza Serikali kuboresha machimbo hayo ili kuongeza uzalishaji wa chumvi, kuongeza mapato ya Serikali na wananchi kupata ajira.