Tangu kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML), ambayo ni kampuni tanzu ya AngloGold Ashanti ilipoanzishwa mwaka 2000 nchini Tanzania, imekuwa kampuni kinara katika kuhakikisha jamii inayozunguka mgodi huo inanufaika kutokana na uwepo wa shughuli za uchimbaji katika eneo hilo.
Lengo la kimkakati la kampuni ya Geita Gold Mining Limited limejikita katika kuhusianisha shughuli za uchimbaji katika sera za maendeleo ya wana-Geita na Tanzania kwa ujumla kuanzia ngazi ya mitaa, kata, wilaya, mkoa, kitaifa na kikanda.
Ndio maana kwa miaka mingi wadau wakubwa wa sekta ya madini katika tasnia hiyo wamejikita kutoa mchango wao katika huduma za kijamii kama vile afya, elimu, miundombinu ya barabara na ujasiriamali.
Mwaka 2018, GGML ilikuwa kampuni ya kwanza ya uchimbaji madini nchini Tanzania kutekeleza mpango wa uwajibikaji wa kampuni kwa jamii (CSR) kwa kuzingatia kifungu cha 105 cha Sheria ya madini namba saba iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2017. Sheria hiyo iliboresha sheria ya madini namba 14 ya mwaka 2010.
Kwa kuwa GGML inakusudia kuzingatia matakwa ya marekebisho ya sheria hiyo ya madini na kuunga mkono juhudi za Serikali katika kujenga uchumi endelevu unaoweza kudumu hata baada ya mgodi kumaliza shughuli zake, tangu wakati huo, Kampuni inawekeza Sh bilioni 9.2 kila mwaka kufadhili miradi ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi mkoani Geita.
Mwaka 2022/2023 pekee,GGML imetoa zaidi ya Sh bilioni 19 hii ikiwa ni katika kusaidia maendeleo ya kiuchumi, kielimu, kiafya, miundombinu na hata huduma za maji.
ELIMU
Kwa kuwa GGML inaamini moja ya nguzo muhimu katika kusukuma gurudumu la maendeleo ya serikali kwa wananchi wake ni elimu, kwenye sekta hii GGML imeunga mkono ujenzi wa shule kadhaa za sekondari na msingi.
Kwa kushirikiana na Halmashauri ya Mji wa Geita, imefanikisha ujenzi wa Shule ya wasichana ya Nyankumbu ambayo ujenzi wake uligharimu zaidi ya Sh bilioni 15 na kuanza usajili wa wanafunzi mwaka 2014.
Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Georgia Mugashe anasema Nyankumbu imekuwa mkombozi kwa mkoa huo na hata mwaka huu wa masomo imesajili wanafunzi wapya wa kidato cha kwanza 240 huku ikishindwa kuchukua wengine kutokana na wingi wa maombi.
Lakini pia kwa kuwa mkoa wa Geita haukuwa na shule nyingi sekondari za kidato cha tano na sita za bweni , mbali na Nyankumbu pia GGML imeshiriki ujenzi wa shule za kwanza za serikali za kidato cha tano na sita katika halmashauri ya wilaya ya Geita ambazo ni shule za Kamena na Bugando.
Shule hizo mbili zilizoanza usajili wa wanafunzi mwaka 2021/2022, GGML imetoa zaidi ya Sh milioni 287.5 kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya Geita kupitia mpango wa CSR.
GGML KILI CHALLENGE AGAINST HIV & AIDS
Kampeni ya GGM Kilimanjaro Challenge against HIV & AIDS iliyozinduliwa miaka 20 iliyopita, imedhihirisha namna kampuni ya GGML ilivyojikita kushirikiana na serikali kutokomeza janga la VVU/ UKIMWI.
Kampeni hiyo inayoishirikisha pia TACAIDS inalenga kukusanya fedha kwa ajili ya mapambano ya VVU/Ukimwi, inashirikisha wapanda mlima Kilimanjaro kwa kutumia baiskeli na miguu hadi kwenye kilele cha mlima huo mrefu barani Afrika.
Tangu mwaka 2002, zaidi ya watu 800 kutoka maeneo mbalimbali duniani, wamepanda mlima huo na kuchangia zaidi ya Sh bilioni 1.3 ambazo zimesaidia taasisi binafsi zaidi ya 20 zinazotoa huduma kwa waathirika wa janga hilo.
Mojawapo ya wafaidika wa fedha hizo ni Kituo cha AGAPE kilichopo mkoani Njombe ambacho msimu uliopita kilipata ruzuku ya Sh. milioni 29.9 kutokana andiko walilowasilisha kwenye timu ya wataalam wa GGM Kili Challenge.
Mratibu wa Kituo, Enara Nyagawa anasema fedha hizo zimewasaidia kuboresha mazingira ya upatikanaji wa elimu kwa watoto na familia zinazoishi na VVU.
KITUO CHA WATOTO YATIMA- MOYO WA HURUMA
Kupitia kampeni hiyo ya Kili Challenge, GGML kwa kushirikiana na Dayosisi ya Kanisa Katoliki Geita, inaendesha kituo cha watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu cha Moyo wa Huruma. Kituo hicho kilichoanzishwa mwaka 2004, kilianza rasmi shughuli zake mwaka 2006.
Kituo hicho ambacho pia kinaendeshwa kwa ushirikiano na Halmashauri ya wilaya ya Geita na Mji wa Geita, kinahudumia watoto 113 na kuajiri wafanyakazi 14 hadi sasa hutumia zaidi ya Sh milioni 50 kila robo ya mwaka kama mishahara huku mahitaji muhimu ya elimu kwa watoto hao ikigharimu zaidi ya Sh milioni 150.
AFYA
Katika sekta ya afya, GGML imewekeza kwa kiasi kikubwa kupitia miradi hiyo ya CSR kwa kutoa misaada katika vituo zaidi ya 20 vya afya vilivyopo mkoani Geita.
Baadhi ya vituo hivyo ambavyo hupatiwa mahitaji mbalimbali ikiwamo vifaa tiba ni pamoja na Nyamalembo, Nyakahongola, Kasota, Kakubiro, Bukoli na Katoro.
Mathalani zaidi ya Sh milioni 565 zimetolewa na GGML kwa hospitali ya rufaa ya Geita na kusaidia kufanya ukarabati wa hospitali hiyo iliyojengwa mwaka 1957 pamoja na kusaidia kuiboresha hospitali hiyo kutoa huduma za moyo.
Katika afya pia GGML imeshirikiana na taasisi ya Rafiki Surgical Mission kutoka Australia ambapo kwa kipindi cha miaka 20 imetoa misaada ya gari nne za kubeba wagonjwa na kutoa ufadhili kwa wagonjwa zaidi ya 2000 waliofanyiwa upasuaji wa mdomo sungura pamoja na wenye majeraha ya moto.
Mmoja wa wagonjwa aliyekuwa na jeraha la moto, Doto Said anaishukuru GGML kwa msaada huo pamoja na madaktari wa Sekou Toure ambao walimpandikiza ngozi kwenye jeraha lake na kumuwezesha kurudisha tabasamu upya.
Mashua tiba (Jubilee boat)
Katika kuhakikisha wananchi wa kanda ya ziwa hususani mikoa ya Geita, Mwanza na Kagera wanapata huduma za afya kwa urahisi, mwaka 2015 GGML kwa kushirikiana na taasisi ya Vine Trust ya nchini Scotland pamoja na Kanisa la African Inland la Geita, waliingia makubaliano ya kutoa huduma za afya kupitia boti maalumu kwa wakazi wa ukanda huo.
Tangu mashuahiyo inayotoa huduma mbalimbali za matibabu, zaidi ya wananchi 158,000 wamenufaika na mashua hiyo inayotoa huduma katika visiwa mbalimbali vilivyopo kwenye Ziwa Victoria kwa siku 14 kisha kurejea Mwanza kwa ajili ya kuweka mafuta. Oktoba 4 mwaka 2021 GGML iliongeza muda wa mkataba.
MAENDELEO YA BIASHARA KWA WATANZANIA
Katika kuzingatia matakwa ya mabadiliko ya sheria ya madini iliyofanyiwa marekebisho 2017, GGML imekuwa ikitoa zabuni kwa wafanyabiashara wa ndani au wazawa ili kutekeleza mpango wa uwajibika wa kampuni kwa jamii.
Kwa kushirikiana na Baraza la Uwezeshaji wananchi Kiuchumi (NEEC), GGML imetoa mafunzo ya masuala ya manunuzi na biashara kwa ujumla ili kupata zabuni za kampuni hiyo kubwa nchini kwa watanzania 300. Hali hiyo imesaidia watanzania kupata zaidi ya asilimia 76 ya zabuni za kampuni hiyo na kuongeza mnyororo wa biashara kati ya GGML na Watanzania.
Akizungumzia mafanikio ya mafunzo hayo, Meneja wa Kampuni ya Blue Coast Investment Limited ambayo ni mmoja wa wakandarasi waliopata zabuni kutoka GGML, Jeremiah Musa, alisema wamefanikiwa kupata zabuni mbili kutoka GGML ambazo ni kusambaza mafuta pamoja na kusafirisha wafanyakazi wa kampuni hiyo.
“Mbali na kusafirisha asilimia 30 ya mafuta ndani ya GGML pia wametupatia mafunzo mbalimbali jambo ambalo limetusaidia kampuni yetu kukua kwa haraka na kupata fursa ya kujitanua na kutoa fursa za ajira kwa Watanzania kwani mpaka sasa tuna wafanyakazi 400 walioajiriwa,” anasema.
MRADI WA IMTT
Vivyo hivyo, katika kuinufaisha jamii ya Watanzania, GGML inatekeleza mradi wa Mafunzo Jumuishi ya Ujuzi kwa Ajili ya Sekta ya Madini (Integrated Mining Technical Training-IMTT) unaolenga kuongeza nguvu kazi kwenye sekta hiyo ya madini.
Mafunzo hayo, hutolewa na Chuo cha Mafunzo ya ufundi stadi VETA- Moshi ambapo kwa kipindi cha mwaka 2021 pekee, GGML ilitoa zaidi ya Sh milioni 132.
UWEZESHAJI WAKULIMA
Kwa upande wa kilimo, GGML kwa kushirikiana na Taasisi ya Kilimo Cholima mwaka 2015 waliendesha programu maalum ya kuwajengea uwezo wakulima wa Nungwe na Bugulula namna ya kulima mazao hayo kisasa. Mafunzo hayo yaliwafikiwa wakulima wa vijiji saba ambao walianzisha kilimo biashara cha alizeti na mpunga.
Katika kipindi cha miaka sita tangu mradi huo uanze, maisha ya wakulima 220 wanaolima hekta 350 za ardhi yamebadilika na kuwa bora kutokana na ufadhili huo wa GGML ambao umewawezesha kupata mashine za kukoboa mpunga na kukamua mafuta ambapo katika mradi huo jumla ya wakulima 700 ambao unajumuisha asilimia 85 ya wanawake, wanalima hekta 600.
Kutokana na elimu waliyoipata pamoja na matumizi bora ya ardhi walifanikiwa kupata mavuno zaidi ya asilimia 250 ya mategemeo Mageuzi hayo yanadhibitishwa na mmoja wa wakulima wa alizeti katika Kijiji hicho cha Kasota, Saa Kumi Makungu ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama cha ushirika cha NYABUSAKAMA.
“Tunawashukuru uongozi wa GGML na halmashauri kwa kutuunga mkono kwa sababu tulikuwa tunatembea umbali wa kilomita 25 kufuata mashine ya kukamua alizeti lakini sasa tunakamulia hapa karibu vivyo hivyo kwa mpunga,” anasema.