Rais wa Kenya, William Ruto amesema Serikali yake inakusudia kuendeleza ujenzi wa bomba la gesi linalounganisha jiji kuu la Tanzania, Dar es Salaam, na mji wake wa pwani wa Mombasa na kuendelea hadi mji mkuu wa Nairobi, katika jitihada za kupunguza gharama za nishati.
Rais Ruto ameyasema hayo wakati akizungumza na vyombo vya habari Ikulu jijini Dra es Salaam, muda mfupi baada ya kufanya mazungumzo na Rais Samia Suluhu Hassa katika ziara yake ya kwanza nchini tangu aingie madarakani mwezi Septemba, 2022.
Mradi huo unatarajia kupunguza gharama za kawi katika sekta ya viwanda, pamoja na familia zilizo majumbani mwao, huku Bomba hilo la urefu wa km 600 likikadiriwa kugharimu karibu dola 1.1 bilioni ambazo ni sawa na pauni 990 milioni.
Mei mwaka jana (2022), mtangulizi wa Ruto, Uhuru Kenyatta na Rais Samia walitia saini makubaliano ya awali ya kusafirisha gesi kutoka Tanzania hadi Kenya, kwa ajili ya kuzalisha umeme, kupika na kupasha joto.
Makubaliano hayo, yalikuwani sehemu ya mpango wa muda mrefu wa kuendeleza miundombinu kati ya mataifa haya mawili yenye uchumi mkubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki.