Wizara ya Afya nchini Somalia, imesema ukame uliolikumba eneo la pembe ya Afrika, unaweza kusababisha vifo 135 kwa siku katika kipindi cha mwezi Januari na Juni 2023, madai ambayo yametolewa pia na Shirika la Afya Duniani WHO, na UNICEF kupitia taarifa yao kwa jamii.
Hatua hii inakuja baada yataarifa ya mapema mwezi huu (Machi, 2023), Shirika la Afya Duniani (WHO) kuonya kuwa karibu watu 100,000 nchini Somalia wanakabiliwa na viwango vya juu vya janga la njaa kutokana na ukame mbaya zaidi kuwahi kulikumba eneo hilo katika miongo minne.
Matokeo ya utafiti yalitolewa Jumatatu (Machi 20, 2023), yalitumia vigezo vya takwimu kukadiria kuwa hadi Wasomali 135 wanaweza kupoteza maisha yao kutokana na sababu zinazohusiana na ukame kila siku katika miezi sita ya kwanza ya mwaka huu, huku jumla ya vifo vikikadiriwa kuwa kati ya 18,100 na 34,200.
Utafiti huo ulitanabaisha kuwa, hali mbaya ya hewa huenda ilisababisha vifo vya watu 43,000 mwaka jana (2022), ikilinganishwa na ukame wa 2017, huku watoto walio chini ya umri wa miaka mitano wakiwa nusu ya waathiriwa.