Aliyewahi kuwa Mbunge wa jimbo la Bunda Mjini, Stephen Wasira amesema kuwa mazingira ya uchaguzi ya mwaka 2015 katika jimbo hilo yalitawaliwa na vitendo vya rushwa iliyosababisha Ester Bulaya kushinda uchaguzi huo.

Akizungumza wiki hii, Wasira amedai kuwa rushwa ilikuwa kila eneo la uchaguzi wa ubunge wa jimbo hilo, kuanzia ngazi ya mpigisha kura hadi kwa msimamizi wa uchaguzi.

Amesema kuwa kutokana na mazingira hayo, hata Malaika angegombea dhidi ya Bulaya katika kipindi hicho asingeshinda

“Kulikuwa na hujuma kubwa sana, kulikuwa na rushwa za kuanzia kwa msimamizi wa uchaguzi mpaka mpigisha kura wa kituo, hata ungepeleka Malaika mwaka 2015 asingeshinda,” Wasira ameiambia Wasafi FM.

Wasira ambaye ni mmoja kati ya wanasiasa wakongwe na nguli nchini, ambaye pia amewahi kuwa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika katika Serikali ya Awamu ya Nne, amesema kuwa anagombea tena ubunge wa jimbo hilo mwaka huu.

Mwanasiasa huyo ameeleza kuwa Julai 14, 2020 ataenda kuchukua fomu ya kukiomba Chama Cha Mapinduzi kumpitisha kuwa mgombea ubunge wa jimbo hilo.

Wasira alipinga mahakamani matokeo ya Ubunge wa Jimbo la Bunda Mjini. Hata hivyo, Bulaya alishinda kesi hiyo ya uchaguzi.

DAS wa Handeni afariki kwenye ajali Dodoma, Mbunge ajeruhiwa
Sita kuamua Simba Vs Young Africans