Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Angellah Kairuki amepiga marufuku tabia ya baadhi ya watendaji wa Serikali kuwa na kampuni binafsi za ujenzi, kwani kufanya hivyo ni kinyume na maadili ya utumishi wa umma na husababisha mgongano wa kimaslahi.
Kauli hiyo ameitoa hii leo Februari 20, 2023 katika Mkutano wa siku moja wa Wahandisi wa Sekretarieti za Mikoa, Mameneja wa Mikoa na Wilaya wa TARURA na Wakuu wa Idara za Miundombinu na Maendeleo Vijijini na Mijini kwenye mamlaka za serikali za Mitaa , uliyofanyika Mtumba jijini Dodoma.
Amesema, “Mtu huwezi kujichukulia hatua mwenyewe hivyo kwa yeyote mwenye kampuni binafsi ya ujenzi ajichunguze itamletea mgogoro mkubwa na sisi kama Serikali hatuwezi kumvumilia Mtumishi wetu ambaye anakiuka kwa makusudi sheria ya maadili ya utumishi wa umma,”
“kuwa na kampuni binafsi inasababisha mgongano wa kimaslahi hivyo ni ngumu sana kufanya kazi kwa ufanisi na kuzingata mkataba kwani wewe ndio kila kitu hilo halivumiliki na unakwamisha malengo ya serikali kuwafikishia wananchi maendeleo,” ameongeza Waziri Kairuki.
Aidha, amewataka watumishi hao kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kwa ufanisi hasa kusimamia fedha zote zinazopelekwa katika halmashauri zitumike kwa wakati na kuzingatia thamani ya fedha ili kuweza kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Kairuki pia amewaagiza TARURA kuwakata gharama wakandarasi wanaochelewesha ukamilishwaji wa miradi na wanaokwenda kinyume na mikataba pasipo na sababu za msingi kwani wanachelewesha huduma iliyokusudiwa kwa wananchi.