Takriban Watu 22 wamefariki kwa ajali baada ya Basi na Lori kugongana kaskazini mwa Senegal, ambapo wafanyakazi wa zima moto wamesema ajali hiyo inatokea ikiwa ni wiki moja baada ya ajali kati ya mabasi mawili pia kugongana na kusababisha vifo vya watu 40.
Mfanyakazi wa Idara ya Kitaifa ya Zimamoto, Papa Ange Michel Diatta amesema ajali hiyo ilitokea karibu na eneo la Sakal lililopo mji wa Louga ambapo zaidi ya watu 20 walijeruhiwa na
Waziri Mkuu, Amadou Ba ameapa kuimarisha sheria mpya za barabarani.
Ba amewaambia Waandishi wa Habari kuwa basi hilo lina uwezo wa kubeba abiria 32, lakini lilikuwa limebeba watu 47, huku Rais wa Senegal, Macky Sall aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kwamba “Ajali nyingine mbaya kwenye barabara zetu.” huku akisema idadi hiyo ya vifo inaonyesha umuhimu wa kuimarisha sheria za usalama wa barabarani.
Inadaiwa kuwa, ajali za barabarani ni jambo la kawaida nchini Senegal, hasa kutokana na uzembe wa madereva, barabara mbovu na uchakavu wa magari, na hivi karibuni nchi hiyo iliingia kwenye siku tatu za maombolezo kufuatia ajali ya mabasi mawili kugongana Januari 8, 2023 katika eneo la katikati la Kaffrine, na kusababisha vifo vya watu 40 na zaidi ya 100 kujeruhiwa.