Kiongozi mkuu wa kanisa katoliki duniani ambaye pia ni kiongozi mkuu wa Vatican, Papa Francis amewasili nchini Kenya leo majira ya saa kumi jioni na kupata mapokezi makubwa na ya heshima.

Papa Francis alipokewa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta na Rais Uhuru Kenyatta na viongozi wengine wakubwa wa dini na serikali na kuelekea katika Ikulu ya nchi hiyo. Kiongozi huyo alipigwa mizinga 21 kama ishara ya heshima kwa kiongozi mkubwa wa Vatican.

Kiongozi huyo alilihutubia taifa hilo akiwa ikulu ya Nairobi ambapo aliwashukuru kwa mapokezi makubwa na ya heshima na kuwasisitiza kuhusu umuhimu wa amani na kuwajali masikini.

Pope 1

“Nawahimiza kuwajali maskini, ndoto za vijana, na kugawana vyema maliasili na nguvu kazi ambazo Mungu amelipa taifa lenu. Nawahakikishia kuendelea kwa juhudi za kanisa Katoliki, kupitia kazi zake za elimu na kusaidia jamii, kutoa mchango katika hili,” alisema Papa Francis.

Aidha, Papa Francis aliwahimiza kuzingatia demokrasia na kutenda mema katika kila wanachokifanya pamoja kuishi kwa uwiano, kuvumiliana na kuheshimiana.

Pope 4

“Jamii zetu zinapoendelea kukumbwa na migawanyiko ya kikabila, kidini au kiuchumi.. binadamu wote wenye nia njema wameitwa kufanyia kazi maridhiano, msamaha na uponyaji. Katika juhudi za kuunda mfumo wa demokrasia, kuimarisha utangamano na uwiano, kuvumiliana na kuheshimiana, lengo kutenda mema linafaa kuwa ndilo kuu,” aliongeza.

 

Papa Francis ataendesha ibada ya misa takatifu kesho nchini Kenya ambapo maelfu ya watu wanatarajiwa kuhudhuria. Serikali ya Kenya imeitangaza Alhamisi (Kesho) kuwa siku ya mapumziko kutokana na ziara hiyo.

 

Mtatiro Aikosoa kwa nukuu ya sheria, Amri ya Makonda kuwaweka selo maafisa waliochelewa kazini
Thomas Muller Ajiweka Kwenye Kumbukumbu Ulaya